Punde kabla ya uchaguzi wa urais na wabunge nchini Liberia, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afŕika Maghaŕibi (ECOWAS) na Umoja wa Mataifa (UN) ziliungana kuendeleza amani, umoja na ushirikishwaji nchini humo.
Ujumbe wa pamoja unaoongozwa na Prof Attahiru Muhammadu Jega - Mkuu wa Ujumbe wa Wachunguzi wa ECOWAS wa uchaguzi nchini Liberia, na Leonardo Santos Simão, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Afrika Magharibi na Sahel (UNOWAS) ulizuru Liberia kabla ya uchaguzi wa mnamo tarehe 10 Oktoba 2023 ili kushirikiana na wadau na kutoa wito wa amani katika kipindi cha uchaguzi.
Katika ziara yao, wajumbe hao walishirikiana na wadau wa siasa, taasisi za kitaifa, wajumbe wa Kikosi cha Wanadiplomasia na Kundi la Nchi la Umoja wa Mataifa. Walitambua hatua iliyopigwa katika maandalizi ya uchaguzi huo, wakisisitiza umuhimu wa kufanya uchaguzi wa kuaminika, wa uwazi na jumuishi.
Wakitoa maoni yao kuhusu matukio ya hivi majuzi ya ghasia za uchaguzi, haswa matukio ya kusikitisha huko Foya katika Kaunti ya Lofa tarehe 29 Septemba, wajumbe walishutumu vitendo kama hivyo na kutaka uchunguzi wa haraka na uwajibikaji kufanywa.
Walisisitiza kuwa "ghasia hazina nafasi katika mchakato wa kidemokrasia" na kuwataka "wahusika wote wa kisiasa kuziepuka na kulinda amani na uwiano wa kitaifa la Liberia".
Ujumbe huu wa pamoja ulihimiza vyama vya kisiasa na wagombeaji wote kushikilia ahadi yao ya uchaguzi wa amani na kutafuta suluhisho mahakamani iwapo kutatokea mzozo, kulingana na kanuni zilizoelezwa katika Azimio la Mto Farmington 2023.
Zaidi ya hayo, walitoa wito kwa watu wa Liberia na viongozi wao kuzingatia maadili ya uvumilivu na amani katika kipindi hiki muhimu cha kuimarisha demokrasia.
Akizungumiza kuhusu ujumbe huo wa pamoja, Bw. Simão alielezea matumaini kwamba wananchi wa Liberia watajitahidi kulinda amani.
Kwa sasa taifa hili lina amani na uthabiti, na linakumbatia demokrasia ambayo imekuwa nguvu inayoliongoza tangu kipindi cha ghasia hapo awali.
Juhudi za pamoja za ECOWAS na Umoja wa Mataifa kabla ya uchaguzi ni thibitisho la moyo wa ushirikiano wa kuunganisha mataifa kwa lengo moja: Afrika inayojulikana kwa amani ya kudumu, umoja miongoni mwa watu wake, na ustawi.
- Wafuatao walichangia makala haya:
- Christiana Solomon (Mshauri wa Amani na Maendeleo, RCO Liberia)
- Marline Bos (Afisa wa Mawasiliano ya Kanda, DCO Africa)
- Oumar Kane (Afisa Mwandamizi wa Masuala ya Kisiasa wa UNOWAS), na
- Gradiah Walker Bou Hussein (Afisa wa Mawasiliano wa Liberia, RCO)