Sorry, you need to enable JavaScript to visit this website.
Skip to main content

Shinikizo la damu: Ripoti ya kwanza ya Shirika la Afya Duniani inaelezea athari mbaya za shinikizo la damu na njia za kuizuia

Kiswahili

Shinikizo la damu: Ripoti ya kwanza ya Shirika la Afya Duniani inaelezea athari mbaya za shinikizo la damu na njia za kuizuia

Karibu mtu mmoja kati ya watatu duniani kote anaishi na shinikizo la damu la 140/90 mmHg, ambalo linaweza kusababisha kiharusi, mshtuko wa moyo, moyo kushindwa kufanya kazi, uharibifu wa figo, na mengine.
2023-09-19
First WHO report details devastating impact of hypertension and ways to stop it.
.
Shinikizo la damu: Ripoti ya kwanza ya Shirika la Afya Duniani inaelezea athari mbaya za shinikizo la damu na njia za kuizuia
WHO / Martha Tadesse
  1. Play Shinikizo la damu: Ripoti ya kwanza ya Shirika la Afya Duniani inaelezea athari mbaya za shinikizo la damu na njia za kuizuia

Pause

Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitoa ripoti yake ya kwanza kabisa kuhusu athari mbaya duniani za shinikizo la damu, pamoja na mapendekezo ya njia za kukabiliana na kisababishi hiki cha vifo. 

Ripoti hii inaonyesha kuwa takriban watu 4 kati ya 5 walio na shinikizo la damu hawajatibiwa vya kutosha, lakini nchi zikiweza kuimarisha matibabu, vifo milioni 76 vinaweza kuepukwa kati ya     mwaka wa 2023 na 2050. 

Shinikizo la damu huathiri mtu mzima 1 kati ya 3 duniani kote.  Hali hii inayotabuliwa kusababisha vifo pia husababisha kiharusi, mshtuko wa moyo, moyo kushindwa kufanya kazi, uharibifu wa figo na matatizo mengine mengi ya afya.

Idadi ya watu wanaoishi na shinikizo la damu (shinikizo la damu la 140/90 mmHg au zaidi au wanaotumia dawa za shinikizo la damu) iliongezeka maradufu kati ya 1990 na 2019, kutoka milioni 650 hadi bilioni 1.3. 

Karibu nusu ya idadi ya watu walio na shinikizo la damu ulimwenguni kote hawajui hali zao. Zaidi ya robo tatu ya watu wazima wenye shinikizo la damu wanaishi katika nchi zenye mapato ya chini na kati.

Uzee na maumbile yanaweza kuzidisha hatari ya kupata shinikizo la damu, lakini vihatarishi vingine kama vile kula chakula chenye chumvi nyingi, kutofanya mazoezi na kunywa pombe kupita kiasi pia kunaweza kuongeza hatari ya shinikizo la damu.

Mabadiliko ya mtindo wa maisha kama vile kula lishe bora, kuacha tumbaku na kufanya mazoezi kunaweza kusaidia kupunguza shinikizo la damu. Baadhi ya watu wanaweza kuhitaji dawa za kudhibiti shinikizo la damu kwa ufanisi na kuzuia matatizo yanayohusiana nayo. 

Uzuiaji, ugunduzi wa mapema na udhibiti madhubuti wa shinikizo la damu ni miongoni mwa mikakati ya gharama nafuu katika huduma za afya na zinapaswa kupewa kipaumbele na nchi kama sehemu ya mwongozo wa kitaifa wa manufaa ya afya unaotolewa katika ngazi ya huduma ya msingi. 

Manufaa ya kiuchumi ya programu zilizoboreshwa za matibabu ya shinikizo la damu huzidi gharama kwa takriban 18 hadi 1. 

"Shinikizo la damu linaweza kudhibitiwa ipasavyo kwa kutumia taratibu rahisi ya dawa za bei nafuu, na bado ni mtu mmoja tu kati ya watano walio na shinikizo la damu ambaye ameweza kulidhibiti." Alisema Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani. "Programu za kudhibiti shinikizo la damu zinasalia kupuuzwa, kutopewa kipaumbele na kukosa ufadhili. Kuimarisha udhibiti wa shinikizo la damu lazima iwe sehemu ya safari ya kila nchi kuelekea huduma ya afya kwa wote, kwa kuzingatia mifumo ya afya inayofanya kazi vizuri, yenye usawa na thabiti, iliyojengwa juu ya msingi wa huduma ya afya ya msingi."

Ripoti hii itazinduliwa wakati wa Kikao cha 78  cha Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambacho kinashughulikia hatua ya Malengo ya Maendeleo Endelevu yakiwemo malengo ya afya kuhusu kujitayarisha na kukabiliana na janga hili, kukomesha kifua kikuu na kufikia Huduma ya Afya kwa Wote. 

Uzuiaji bora na udhibiti wa shinikizo la damu utakuwa muhimu kwa maendeleo katika haya yote. 

Kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa wanaotibiwa ipasavyo kwa shinikizo la damu hadi viwango vinavyozingatiwa katika nchi zilizofanya vizuri kunaweza kuzuia vifo milioni 76, viharusi milioni 120, mshtuko wa moyo milioni 79, na visa milioni 17 vya moyo kushindwa kufanya kazi kuanza sasa hadi mwaka wa 2050.

"Mashambulio mengi ya moyo na kiharusi duniani hii leo yanaweza kuzuiwa kwa dawa za bei nafuu, salama, na mikakati mingine, kama vile kupunguza kula chumvi," alisema Michael R. Bloomberg, Balozi wa Dunia wa Shirika la Afya Duniani wa Magonjwa Yasiyo Ambukizi na Majeraha. "Kutibu shinikizo la damu kupitia huduma ya afya ya msingi kutaokoa maisha, huku pia kuokoa mabilioni ya dola kwa mwaka."

Shinikizo la damu linaweza kutibiwa kwa urahisi na dawa salama, zinazopatikana kwa wingi na za bei nafuu kwa kutumia programu kama vile HEARTS

Mfuko wa kiufundi wa Shirika la Afya Duniani wa HEARTS wa kudhibiti magonjwa ya moyo na mishipa katika huduma ya afya ya msingi na Mwongozo wa dawa za kutibu shinikizo la damu kwa watu wazima utoa hatua zilizothibitishwa na za vitendo ili kutoa huduma bora ya shinikizo la damu katika mazingira ya huduma ya afya ya msingi.

Udhibiti mzuri wa shinikizo la damu katika jamii na nchi nzima unaweza kufikiwa katika nchi za viwango vyote vya mapato. Zaidi ya nchi 40 za mapato ya chini na kati, zikiwemo Bangladesh, Cuba, India na Sri Lanka, zimeimarisha huduma zao za shinikizo la damu kwa mfuko wa HEARTS, na kuandikisha zaidi ya watu milioni 17 katika programu za matibabu. 

Nchi kama vile Kanada na Korea Kusini ziliwasilisha programu pana za matibabu ya shinikizo la damu, na nchi zote mbili zilipita alama ya asilima 50 ya udhibiti wa shinikizo la damu kwa watu wazima wanaoishi na shinikizo la damu. 

Programu za kitaifa za udhibiti wa shinikizo la damu zilizoendelezwa zinaweza kufanikiwa na kiwango cha juu cha udhibiti wa shinikizo la damu utachangia visa vichache vya kiharusi na mashambulizi ya moyo, na maisha marefu, yenye afya. 

Ripoti hiyo inasisitiza umuhimu wa kutekeleza huduma bora ya shinikizo la damu inayopendekezwa na Shirika la Afya Duniani ili kuokoa maisha, inayojumuisha vipengele vitano vifuatavyo:

  • Taratibu: dozi ya dawa  na taratibu za matibabu mahususi za dawa zenye hatua mahususi za kudhibiti shinikizo la damu lisilodhibitiwa zinaweza kurahisisha huduma na kuboresha uzingatiaji.
  • Usambazaji wa dawa na vifaa: upatikanaji wa mara kwa mara, usiokatizwa wa dawa za bei nafuu ni muhimu kwa matibabu ya shinikizo la damu; kwa sasa, bei za dawa muhimu za kupunguza shinikizo la damu hutofautiana kwa zaidi ya mara kumi kati ya nchi.
  • Huduma zinazojumuisha kundi: matokeo ya mgonjwa huboreka wakati timu inaposhirikiana kurekebisha na kuimarisha dawa za shinikizo la damu kwa maagizo na taratibu za daktari.
  • Huduma zinazomhusu mgonjwa: kupunguza vikwazo vya huduma kwa kutoa dawa ambazo ni rahisi kutumia, dawa za bure na ufuatiliaji wa karibu wa nyumbani na ufuatiliaji wa shinikizo la damu kupatikana kwa urahisi.
  • Mifumo ya taarifa: mifumo inayomlenga mtumiaji, mifumo rahisi ya taarifa huwezesha kurekodi kwa haraka data muhimu ya kiwango cha mgonjwa, kupunguza mzigo wa uwekaji data wa mfanyakazi wa afya, na kusaidia uimarikaji wa haraka huku ukidumisha au kuboresha viwango vya huduma.

“Kila saa, zaidi ya watu 1,000 hufa kutokana na kiharusi na mshtuko wa moyo. Vifo hivi vingi vinasababishwa na shinikizo la damu, na vingi vingeweza kuzuilika,” alisema Dkt. Tom Frieden, Rais & Mkurugenzi Mtendaji, Resolve to Save Lives. "Huduma nzuri ya shinikizo la damu ni nafuu, inaweza kufikiwa, na inaimarisha huduma ya afya ya msingi. Changamoto sasa ni kutoka  kwa “walio katika uwezo wa kufikiwa” hadi “waliofikiwa.” Hi inahitaji kujitolea kwa serijali mbalimbali kote duniani."

Jifunze zaidi kuhusu athari za kimataifa za shinikizo la damu na mfuko wa HEARTS wa kudhibiti hapa.

Soma ripoti kamili hapa.

Shirika la Afya Duniani limeshirikiana na Resolve to Save Lives, shirika lisilo la faida, kusaidia nchi kote ulimwenguni kuandaa mfuko wa uchunguzi wa kiufundi wa HEARTS—mtazamo wa kimkakati, hatua kwa hatua wa kusaidia nchi kuimarisha huduma za shinikizo la damu katika mipangilio ya huduma ya afya ya msingi, ambayo inajumuisha na taratibu za matibabu. Tangu 2017, Bloomberg Philanthropies limesaidia juhudi za kimataifa za kuokoa za Shirika la Afya Duniani na Resolve to Save.

Michael R. Bloomberg, mwanzilishi wa Bloomberg LP na Bloomberg Philanthropies, ndilo Balozi wa Dunia wa Shirika la Afya Duniani kwa Magonjwa yasiyo Ambukizi na Majeraha tangu 2016. Uwekezaji wa Bloomberg Philanthropies katika afya ya umma unajumuisha mipango mikuu, ya kuokoa maisha ili kupunguza tumbaku na utumiaji wa sigara za kielektroniki miongoni mwa vijana kupitia Bilioni 1.58 za Dola za Marekani katika uwekezaji, kusaidia sera ya chakula bora, kupunguza kuzamia majini, na kuboresha usalama barabarani na afya ya uzazi, miongoni mwa mengine.  Mwezi Julai 2022, Bloomberg Philanthropies iliwekeza zaidi milioni 115 za Dola za Marekani katika mpango wake wa Afya ya Moyo na Mishipa - na kufanya jumla ya uwekezaji wake kufikia milioni 216 za Dola za Marekani tangu 2017 - kuendelea kuzuia vifo vinavyosababishwa na ugonjwa wa moyo.

.