Florence Otedola, maarufu kama DJ Cuppy, alizuru makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York wiki hii ili kushiriki katika matukio ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Amani ya mwaka huu, tarehe 21 Septemba. Katika mahojiano na Kingsley Ighobor kutoka Afrika Upya, alijadili juhudi zake za uhisani na kusisitiza kwa nini kila mtoto anastahili elimu. Haya hapa ni madondoo:
Afrika Upya: Kwa nini umefika hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa?
DJ Cuppy: Nina furaha sana kuwa hapa. Jina langu ni DJ Cuppy, anayejulikana pia kama Florence Otedola. Mimi ni DJ wa kimataifa na mwanahisani, lakini muhimu zaidi, mimi ni mtetezi wa Lengo la 4 [elimu bora] na Lengo la 5 [usawa wa kijinsia].
Nilialikwa hapa New York kushiriki katika shughuli za Siku ya Kimataifa ya Amani.
Nilikuwa msichana mdogo wa Nijeria mwenye ndoto za ndani, lakini elimu imenifanya kuwa mwanamke mwenye maono ya kimataifa katika umri wa miaka 30.
Kama unavyojua, makao makuu ya Umoja wa Mataifa yako mbali sana na Lagos nilikozaliwa na mojawapo ya miji yenye shughuli nyingi zaidi barani Afrika. Kitu kimoja kinachonitofautisha na vijana wengi wa Nijeria ni elimu.
Elimu nchini Nijeria inaonekana kama majaliwa, kwa hivyo nina shauku ya kushughulikia changamoto hiyo.
Je, unafanya nini kuhusu changamoto hiyo?
Ninafanya mambo mengi. Nilianzisha Wakfu wa Cuppy miaka sita iliyopita na kufikia sasa tumesaidia zaidi ya wanafunzi 50,000 wa Nijeria kupata elimu.
Uhisani ni uzoefu; hauhusu tu msaada; hauhusu kutoa tu; pia unahusu kujifunza. Moja ya mambo ambayo nimejifunza hadi sasa ni kwamba nilidhani kuwa nilihitaji kutoa tu zana za elimu nchini Nijeria. Kaskazini mwa Nijeria, hasa, wasichana wengi wadogo hawana hata fursa ya kupata elimu. Kwa hivyo, hivi majuzi nilielekeza juhudi zangu kwa majimbo katika mkoa huo, ikiwemo Katsina na Borno.
Wakfu wa Cuppy unafadhili kituo cha kuleta utulivu huko Maiduguri [mji mkuu wa Jimbo la Borno]. Kuna visa vya waasi na ugaidi katika eneo hilo. Kwa bahati mbaya, unapoenda huko, huwezi tu kumpa mtoto mgonjwa kitabu; pia unapaswa kuhakikisha mtoto huyo amepata matibabu.
Je, unawapa vitabu?
La, sivyo. Tulilenga kuwapa vitabu hadi pale tulipogundua kuwa wanahitaji huduma ya afya ya msingi kwanza. Kwa hivyo, hivi ndivyo Malengo ya Maendeleo Endelevu yote yanavyoingiliana. Tukishashughulikia afya zao, tutapiga hatua inayofuata, ambayo ni ya kuwaelimisha.
Lazima uhakikishe kuwa humwekei mtu plasta kwenye jeraha bali unalitibu jereha hilo.
Unashughulika na takriban wanafunzi 50,000, lakini kuna mamia ya maelfu, kama sio mamilioni, wanaohitaji usaidizi. Je, unafanya kazi na washirika wengine, ikijumuisha serikali?
Tuna washirika kadhaa. Huwezi kuifanya hii kazi peke yako. Ni muhimu kuiona serikali kama mshirika. Ni muhimu kushirikiana.
Nitakuwambia ukweli, kuwasaidia watoto hawa katika elimu ni jambo lililo mbali sana na kazi yangu kama DJ, lakini ninataka wengine walio kama mimi wajitokeze kusaidia. Inahusu kupanda mbegu.
Ninajivunia sana kuwa nimefuzu hivi majuzi kutoka Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza. Lakini cheti changu sio amana yangu kuu kutoka chuo kikuu; badala yake, ni Mfuko wa Wakfu wa Cuppy, ambao ni mfuko wa kwanza kabisa katika Chuo Kikuu cha Oxford kwa wanafunzi wa Kiafrika. Wanafunzi wengi ughaibuni wanakosa mahitaji ya kimsingi kama vile mavazi ya msimu wa baridi na uwezo wa kulipa kodi.
Kwa hiyo, tunaangalia taasisi za elimu ya msingi na za juu.
Ninataka tu kila mtoto awe na azma na shauku ya kupata elimu.
Je, mgeuko huo ukoje kwako, kutoka kwa burudani hadi usomi?
Mambo haya yote nayasawazisha. Sidhani kama tunapaswa kuwekwa kwenye kisanduku kimoja.
Sidhani kama DJ hawezi kuleta mageuzi mazuri katika ulimwengu, na sidhani kama mwanahisani hawezi kufanya muziki. Umoja wa Mataifa ni mfano mzuri wa hilo. Sio tu kwamba walinialika kuzungumza, lakini pia walinialika kuja kucheza muziki.
Tuambie kuhusu ushirikiano wako na Umoja wa Mataifa.
Umoja wa Mataifa ni shirika muhimu sana, na ninajivunia kujihusisha na mambo mengi nao. Hivi majuzi, nilitiwa moyo sana na kazi ya UNDP nchini Nijeria. Lazima tuwe na mawazo ya kiulimwengu, lakini lazima pia tuwe na mawazo ya ndani.
Imekuwa hali ya kustaajabisha sana. Ninaweza tu kuwa na matumaini kwamba hali hii itawahimiza watu wa Nijeria kujihusisha na mashirika yote katika Umoja wa Mataifa.
Ilifurahisha kuchezea watu muziki wa kutoka Nijeria hapa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York.
Je, ulipokelewa vipi?
Mapokezi yalikuwa ya kufana sana. Nilicheza wimbo ninaoupenda sana, niliouimba na Zlatan, unaoitwa "Gelato." Ilifurahisha pia kucheza baadhi ya nyimbo za Kiyoruba. Haya yote yalikusudiwa kuonyesha kuwa unaweza kuwa katika tasnia ya muziki na burudani na bado ukawasilisha ujumbe mzuri.
Je, unapanga kufanya nini sasa?
Nataka kuendelea na kazi yangu ya uhisani. Ulimwengu unabadilika, unakuwa bora au mbaya, kwa namna fulani.
Ninafanya mambo kwa makusudi.
Jambo ambalo sasa linanifurahisha zaidi ni kukutana na watu kutoka kote ulimwenguni. Na Umoja wa Mataifa unatoa jukwaa kwa hilo. Unajua, ninafanya ninalolifanya Nijeria, lakini mtu mwingine analifanya nchini India, mtu mwingine analifanya nchini Kanada, au Marekani.
Wakati mwingine, tunapokuwa na siku ambazo hatuhisi kuwa na motisha sana, inalazimu mtu kutulia ili apate mtazamo kuhusu kile tunachoweza kujifunza kutoka kwa watu wengine.
Niliweza kukutana na mwigizaji na mkurugenzi wa filamu kutoka Marekani, Michael Douglas, katika Umoja wa Mataifa. Amefanyia Umoja wa Mataifa kazi nyingi sana na nilipenda ujumbe wake mkuu leo, ambao ni, "Amani inaanza na mimi."
Mwishowe, ni bora kuanza kufanya jambo. Mara nyingi watu huniuliza niliwezaje kutekeleza mengi haya. Lakini unajua, nilianza tu — nikajaribu kufanya kitu. Nilijaribu kuunda wimbo wangu wa kwanza. Nilituma ombi la kuenda shuleni. Niziungumza na mtu fulani.
Mengi ya makuu tunayoyafurahia duniani hutokana na mtu kuchukua hatua hiyo ya kwanza!