Sorry, you need to enable JavaScript to visit this website.
Skip to main content

Misri inajikakamua kukomesha umaskini, njaa kufikia 2027

Kiswahili

Misri inajikakamua kukomesha umaskini, njaa kufikia 2027

Mpango wa nchi hii wa "Maisha yenye Heshima" unashughulikia Malengo yote 17 ya Maendeleo Endelevu, na kusisitiza umuhimu wa mtazamo kamili wa maendeleo ya binadamu.
2023-10-11
a woman.
.
Mpango wa nchi hii wa "Maisha yenye Heshima" unashughulikia Malengo yote 17 ya Maendeleo Endelevu, na kusisitiza umuhimu wa mtazamo kamili wa maendeleo ya binadamu.
UNDP Egypt
  1. Play Misri inajikakamua kukomesha umaskini, njaa kufikia 2027

Pause

Misri imejitolea kukomesha umaskini na njaa kufikia 2027. Katika Mkutano wa Mkuu kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu wa 2023, Misri iliweka ahadi thabiti na halisi za kuharakisha maendeleo yake kuelekea Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu.

Mkutano Mkuu kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu, ulioandaliwa na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York mwezi Septemba, ulipatia nchi nyingi jukwaa la kuonyesha na kuharakisha juhudi zao kwa mustakabali endelevu. 

Muhimu katika ahadi ya Misri ni "Mpango wa Maisha yenye Heshima." Mpango huu wa kina unashughulikia Malengo yote 17 ya Maendeleo Endelevu, ukisisitiza umuhimu wa mtazamo kamili wa maendeleo ya binadamu.

Akizungumza katika Mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Sameh Hassan Shoukry Selim alisisitiza haja ya dhamira ya dharura ya kimataifa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu. 

"Ahadi hii inapata umuhimu zaidi, kwa kuzingatia majanga ambayo yamezuia mwelekeo wetu wa maendeleo," alisema wakati wa kikao kilichoitwa Majadiliano ya Viongozi 1: "Kuimarisha hatua kwenye mabadiliko muhimu ili kuharakisha uafikiaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu."

Bw. Shoukry aliangazia msururu wa ahadi thabiti, akisisitiza kujitolea kwa Misri kwa mpango wake kabambe wa maendeleo - "Ruwaza ya 2030." 

"Misri kwa sasa inashughulikia maendeleo ya watu, haswa kwa kuzingatia elimu, afya, ushiriki wa wanawake katika soko la ajira, pamoja na ushiriki wa sekta binafsi ili kumaliza njaa ifikapo 2027 na kukomesha umaskini kufikia 2027 ,” alisisitiza.

Kabla ya Mkutano Mkuu wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, Wizara ya Mipango na Maendeleo ya Uchumi ya Misri, kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa, ilifanya mashauriano ya kitaifa huko Kairo tarehe 11 Septemba. 

Hafla hiyo ilileta pamoja wawakilishi 80 kutoka kote serikalini, vyombo vya habari, wasomi, na mashirika ya kiraia, ikisisitiza kujitolea kwa nchi katika kufanya maamuzi shirikishi na jumuishi.

"Ahadi mpya za kitaifa na ushiriki wa Misri katika Mkutano wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ni mifano ya dhamira hii katika vitendo. Mashauriano ya kitaifa ya leo na wawakilishi kutoka jamii nzima ya Misri ni hatua muhimu katika kujenga maelewano kuhusu yale yanayofaa kutekelezwa kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu na jinsi kila mtu anavyoweza kuwa na jukumu la kusaidia," alisema Elena Panova, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Misri wakati wa mkutano huo.

Mashauriano haya ni sehemu ya mpango wa kipekee wa ushirikishaji wa wadau wa Misri, ulioandaliwa kwa ushirikiano na Timu ya Umoja wa Mataifa nchini. 

Maoni kutoka kwa mashauriano haya na uchunguzi wa mtandaoni yaliboresha ahadi ya Misri kabla ya Mkutano wa Malengo ya Maendeleo Endelevu. 

Umoja wa Mataifa nchini Misri pamoja na serikali, ulitayarisha Ripoti ya kina kuhusu Mafunzo yanayotokana na Malengo ya Maendeleo Endelevu, ikifahamisha ahadi hizi na kulenga kuharakisha kutimiza.

Hala Elsaid, Waziri wa Mipango na Maendeleo ya Kiuchumi, alisisitiza kujitolea kwa Misri katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu katika ujumbe wake, kusisitiza kukomesha umaskini, na kushughulikia changamoto muhimu, ikiwemo njaa, ukosefu wa usawa, ulinzi wa mazingira, na hatua za mabadiliko ya tabianchi.

"Ahadi ya Misri ya kuchangia juhudi zetu za pamoja za kufikia maendeleo endelevu ilionekana wakati wa uongozi wake wa COP27, ambayo ilipitisha malengo kabambe na yenye mwelekeo wa vitendo, pamoja na Mpango wa Utekelezaji wa Sharm el-Sheikh ambao unajumuisha mafanikio makubwa katika kupunguza, kustahimili na kutoa njia za utekelezaji,” alisema.

Zaidi ya Mkutano wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, Misri inaendelea na mtazamo wake wa kiubunifu kuelekea kufikia malengo haya. 

Mpango wa “Maisha yenye Heshima” unalenga kuimarisha viwango vya maisha katika vijiji vyenye watu maskini kupitia njia mbalimbali, ikijumuisha kuwawezesha wanawake na kuendeleza miundombinu.

Aidha, Umoja wa Mataifa na serikali ya Misri wameungana kikamilifu katika maandalizi ya Mkutano huo. 

Ushirikiano huu unaonyesha kujitolea kwao kwa pamoja kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu, kuhakikisha ulinganifu na mikakati muhimu ya kitaifa kama vile Mkakati wa Kitaifa wa Mabadiliko ya Tabianchi 2050Mkakati wa Kitaifa wa Haki za Binadamu, na Ruwaza ya Misri ya 2030.

Ikionyesha ari yake ya kiubunifu, Misri imechukua nafasi ya mbele katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu. Nchi hii imetayarisha ripoti za utekelezaji kwa kila kaunti, imewasilisha Maoni ya Hiari ya Ndani yenye ufahamu katika Jukwaa la Kisiasa la Ngazi ya Juu la 2023, na hata kuzindua kipimo bora cha kila kaunti. 

Huku Mkutano wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ukifanya kazi kama hatua ya kimataifa kwa nchi kutangaza ahadi zao, safari ya kweli huanza baadaye. Ahadi lazima zibadilishwe kuwa vitendo vinavyoonekana. 

Katika safari hii ya kupiga hatua, Misri haiko peke yake. Umoja wa Mataifa ni mshirika mkuu. Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo Endelevu wa Umoja wa Mataifa (UNSDCF) 2023-27 uliotiwa saini hivi majuzi ni thibitisho la ushirikiano huu, unaowasilisha maono ya pamoja ya mustakabali mwema na endelevu zaidi.

Kama Waziri Shoukry alivyohitimisha jijini New York, "Kwa nia njema ya kisiasa, bado tunayo fursa ya kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu na matarajio tunayoshikilia."

.