Katika kampuni changa yenye nafasi pana iliyoko katikati mwa Luanda, jiji kuu lenye shughuli nyingi la Angola, kundi la vijana wa kiume na wa kike waliokodoa macho na wanaochipukia taaluma wamezama kwenye skrini zao za tarakilishi.
Wanasakura mtandaoni kwa makini kutafuta fursa kubwa inayofuata ya kibiashara, kupata taarifa za mipango yao ya biashara, kufanya utafiti wa soko, au kutathmini hatari wanazokaribia kufanya.
Kinachowaunganisha ni dhamira ya pamoja—kupata mafanikio kama wajasiriamali.
Wanafahamu kuwa barabara ya mafanikio hujengwa kwa bidii. Ndoto zao zinaenea zaidi ya faida ya kibinafsi; wanasukumwa kuchangia maendeleo ya taifa lao na kuinua familia zao.
Vijana hawa wa Angola wanajivunia kuwa na lakabu "empretecos", neno linalotokana na "Empretec" — programu kuu ya kujenga uwezo ya UNCTAD inayolenga kukuza ujasiriamali na kusaidia biashara ndogo ndogo, ndogo na za wastani (MSMEs).
Empretec inatambuliwa rasmi na azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambapo iliitwa "mpango wa mtazamo wa tabia."
Neno "empreteco" linamrejelea mtu yeyote ambaye amepitia mafunzo haya. Kuna takriban empretecos 3,000 wa Angola, wa umri na jinsia tofauti tofauti, na waliotoka sehemu mbalimbali za taifa hilo.
Afrika Upya ilishiriki katika mazungumzo na vijana watano wa empreteco, wakijumuisha wanawake watatu na wanaume wawili. Kuna:
- Laudiana Nicolau, meneja wa kampuni ya mafunzo ya ujasiriamali.
- Wilson Kiteque, mkufunzi mashuhuri wa empretec ambaye amesafiri katika mikoa mbalimbali nchini humo.
- Mara Francisca Kanganjo, mmiliki wa duka la mtandaoni la kuoka mikate na biskuti.
- Antonio Pehehaff Neto, mwanzilishi wa kampuni ya usanifu picha na chapa.
- Carla Gabriel Salvador, mwendeshaji wa duka la vito na vifaa vya mitindo mtandaoni.
Ni nini kilichochea mabadiliko ya ghafla kuelekea ujasiriamali?
"Ni mafunzo ya ujasiriamali tuliyokamilisha hivi majuzi," Bi. Laudiana Nicolau, anajitolea. Kutaka kudhihirisha kuwa wanawake wanaweza kuondokana na hali ya utegemezi, anasisitiza, "Wanawake mara nyingi huwategemea wanaume, kwanza baba yao kama kiongozi wa familia na kisha kuolewa na kuwa wategemezi kwa waume zao kwa kila kitu. Ninataka kuonyesha kuwa vijana wa kike wanaweza kumiliki biashara zenye mafanikio. Mafunzo hayo yalinipa uwezo wa kujiamini na uhuru wa kifedha."
Mara anarejelea hisia za Laudiana, akisisitiza kuwa kuweka na kufuatilia kwa bidii malengo ndio ujumbe wake mkuu kutoka kwa mafunzo hayo.
Carla, ambaye sasa ana ufahamu wa wazi wa fursa za kibiashara, mikakati ya uanuwaishaji, na dhamira isiyoyumba inayohitajika kwa mafanikio, anaahidi, "Sasa nimejitolea kufanya yote niwezayo kwa kila jitihada ninayochagua maishani."
Msisitizo wa mafunzo hayo kuhusu mbinu za udhibiti wa biashara za ndani na nje, kuweka malengo, kuchukua hatari kwa weledi, kujiamini, na stadi za mashauriano madhubuti ndiyo yaliyoangaziwa kwa Wilson, mmoja wa wakufunzi wakuu wa empretec.
Kubahatisha
Mada inayojirudia miongoni mwa empretecos hao ni utayari wao mpya wa kubahatisha kwa weledi—mtazamo ambao hapo awali walikuwa wakiuchukia.
Wilson anakumbuka shauku dhaifu miongoni mwa Waangola wakati mafunzo hayo yalipoanza mwaka wa 2018.
Hata hivyo, kupitia mapendekezo ya kimazungumzo, wale waliomaliza mafunzo hayo walianza kueneza habari, na kusababisha kuongezeka kwa mvuto kadri miaka ilivyosonga.
Kuwasikiliza wajasiriamali hawa wanaochipukia kunasisitiza matokeo muhimu zaidi ya mafunzo yao—tumaini lililofanywa upya katika uwezo wao wa kufaulu na kuamsha upya azma ya kuyatimiza malengo yao.
Kuchangia maendeleo ya taifa
"Nataka kuendeleza taifa langu," anasisitiza Laudiana, dhamira yake ikidhihirika.
Maono ya Antonio yanaenea zaidi: "Ninalenga kuinua jamii yangu, kusaidia marafiki na familia yangu. Sijali kuuhusu utajiri wangu wa kibinafsi; ninataka kukumbukwa kama mtu ambaye aliathiri vyema maisha wakati nimeondoka."
Matarajio yao ya kibinafsi yanadhihirisha ukomavu wa ajabu ambao unakinzana na umri wao, wengi wao wakiwa katika miaka yao ya 20. Habari njema kwao ni kwamba mafunzo hutoa njia wazi ya mafanikio, na wanaweza kufikia mtandao, rasilimali muhimu ya kuendelea kupata akili ya biashara.
"Katika mazingira ya biashara ya leo, maarifa ni nguvu," anasisitiza Wilson, akisisitiza kwamba hamu kubwa ya mafunzo inathibitisha hamu miongoni mwa Waangola kwenda zaidi ya mafuta na gesi na kutegemea serikali kwenda kwa sekta mbalimbali ambapo watu binafsi wanaweza kufaulu.

Antonio anaeleza kuwa mafunzo hayo ni ya vitendo sana huku akisisitiza jinsi alivyojionea wakati wa mafunzo hayo namna biashara inavyoweza kupata faida.
"Lilikuwa ni jaribio la kweli. Tuliunda vikundi, na kikundi changu kilianzisha kampuni ya usambazaji wa sharubati. Mara moja tulianza kuwafikia wateja watarajiwa na ndani ya siku tatu tulikuwa tumeuza takribani Kwanza 170,000 za Angola (takriban $200). Ilikuwa ajabu sana," anakumbuka.
Anasema kuwa yu sasa tayari kutumia dhana alizojifunza katika biashara yake binafsi, akilenga kutambulika kitaifa na kimataifa ndani ya miaka mitano ijayo.

Changamoto mbele
Hata hivyo, bighairi ya fursa nyingi katika uchumi ambao kawaida unatawaliwa na tasnia ya uziduaji, empretecos wanazitambua changamoto watakazokabiliana nazo.
Hizi ni pamoja na uchumi unaoimarika kutokana na janga la COVID-19, sarafu inayobadilikabadilika ambayo inafanya tathmini ya hatari isitabirike, na kusita kwa benki kutoa mikopo kwa wajasiriamali wachanga wasio na rekodi zilizowekwa.
Mara anasema pia anakabiliana na ushindani mkubwa kutoka kwa makampuni yaliyoimarika katika tasnia yake, akisema, "Nimezifanya hesabu na kushangaa ni kwa nini wanatoa bei ya chini, ikizingatiwa tunatumia vifaa sawa." Akiuelezea ushindani huo kama usio wa haki, anatumai kuukabili kwa kufafanua upya soko analolenga
Laudiana anaamini kuwa kuna haja kubwa ya kubadilisha mawazo ya watu kuhusu ujuzi wa kifedha. Anasema hivi: “Watu wanastahili kuanza kuelewa jinsi pesa zinavyofanya kazi. Kutasaidia.”
Jambo la msingi kwa Wilson ni mazingira ya kiuchumi, akisisitiza kwamba ujasiriamali unahitaji sera za usaidizi ili kustawi.
Hata hivyo, sehemu ya mpango wa UNCTAD wa Kufanya Mageuzi kwa Manufaa ya Biashara (Transforming4Trade) ni pamoja na kuchunguza sera za sasa na kupendekezea serikali sera zinazostahili kupewa usasa katika sekta mbalimbali, na kuweka mazingira wezeshi kwa ujasiriamali kustawi.
Empretecos wanaporejea kwenye tarakilishi katika vituo vyao vya kazi bada ya mazungumzo yetu, Wilson ana ujumbe mmoja wa mwisho: "Tafadhali uwasilishe ujumbe huu kwa kila mtu, kwamba mafunzo haya yanapaswa kufanywa kuwa ya lazima kwa kila kijana nchini Angola na kote Afrika. Tunahitaji kubadilisha hatima ya bara hili. "