Paul Akiwumi, Mkurugenzi wa Kitengo cha Afrika, Mataifa yanayoendelea na Programu Maalumu katika Shirika la Biashara na Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNCTAD), alizuru jijini New York mwezi wa Septemba kuendeleza Mkakati wa Athari ya Juu, wa shirika lake Transforming4Trade. Kingsley Ighobor kutoka Afrika Upya alijadili mkakati huu na manufaa yake kwa nchi za Afrika na Bw. Akiwumi. Hiya hapa ni madondoo ya mazungumzo yao:
Ulisafiri hadi New York, kwa ajili ya uzinduzi wa Transforming4Trade, mkakati unaolenga kubadilisha miundo ya kibiashara na kiuchumi ya Afrika. Je, unaweza kutufahamisha zaidi kuhusu mkakati huo?
Ili kushiriki katika biashara ya kimataifa, nchi lazima iendelee kuzalisha bidhaa au huduma bora zaidi na za kiteknolojia. Mkakati huo unajikita katika kufikia mageuzi ya kimuundo kupitia mkabala kamilifu wa maendeleo ya kiuchumi, sio kupitia miundo ya kitamaduni kama vile bidhaa au utegemezi wa kisekta.
Tukio hili liliangazia mafanikio ya programu yetu ya majaribio nchini Angola, ambapo tumekuwa tukifanya kazi kwa miaka saba sasa. Tumefanikiwa kusaidia nchi hii kuelekea kwenye lengo lake kuu la maendeleo ya kitaifa la kuinua uchumi kutoka kutegemea mafuta.
Juhudi zetu zimesaidia marekebisho ya sera nyingi, zimesaidia kutambua njia mpya za mseto na kusaidia kikamilifu maendeleo ya mifumo bora ya kuongeza thamani, kuimarisha msaada wa kijasiriamali, kuchunguza mifumo ya thamani ya kikanda na kimataifa, kuboresha uwezo wa mazungumzo ya biashara na kufikia viwango vya kimataifa vya mauzo ya nje, na kusaidiwa na bidhaa za biashara, miongoni mwa mengine.
Zaidi ya hayo, tumechangia kuunda sera mpya za uwekezaji na viwanda zinazounganisha vipengele hivi muhimu.
Ukuzaji wa miundombinu ni muhimu, tunapofanya kazi ili kuunda viungo muhimu vya usafiri kwa ajili ya kuunganisha sekta mbalimbali kama vile sekta ya kilimo na viwanda pamoja na usindikaji.
Kwa nini ulichagua kuonyesha mafanikio ya Angola jijini New York?
Maendeleo ya Angola yanaonyesha matokeo makubwa na athari ambayo inaweza kupatikana kupitia utekelezaji wa mtazamo jumuishi unaotegemea ithibati, na wa sekta mbalimbali wa maendeleo ya kiuchumi, wenye dira ya muda mrefu.
Kwa sasa tunatafuta washirika wapya.
Lengo letu sio tu kuangazia mtazamo wetu, lakini pia kutangaza kwamba hivi majuzi tumezindua mikakati kama hiyo nchini Kenya na Ethiopia.
Pia tuna mipango kwa mataifa ya Msumbiji, Malawi, na Zambia. Kwa hakika, nitakuwa nchini Zambia mwezi wa Oktoba kuzindua mkakati huu huko.
Je, mkakati huu unalenga nchi za Afrika pekee?
La, ni mkakati wa kidunia. Tuna mikakati kwa nchi nyingi kama vile Honduras. Kuimarisha uwezo wa uzalishaji ni jambo linalouhusu ulimwengu wote, na mtazamo wetu wa kijumla unatoa mtazamo uliounganishwa kuhusu maendeleo yanayoleta tija.
Wakati wa hafla hiyo jijini New York, tulipata nchi nyingine zaidi ya 20 zilizofurahishwa na mkakati wetu, kudhihirisha kuwa umaarfu wa mkakati huu.
Lengo letu ni kuwa na idadi kubwa ya nchi zinazoshiriki katika mkakati huu ifikapo 2030.
Je, kuna nchi zozote za Afrika kati ya hizo 20 zinazoonyesha kufurahishwa na mkakati wenu?
Ndiyo, tunapata umaarufu mkubwa kutoka kwa nchi za Afrika, kama Nijeria, ambako tunafanya kazi kwa sasa.
Pamoja na Tathmini ya Kitaifa ya Pengo la Uwezo wa Tija, tunachunguza mtazamo wa kina zaidi nchini Nijeria, tukifanya kazi katika ngazi ya serikali. Kwa kiwango hiki cha maelezo, serikali inaweza kupata maarifa kuhusu uwezo wa uzalishaji wa mataifa binafsi na kulenga sera zake ili kuimarisha uzalishaji wa bidhaa na huduma kwa ufanisi zaidi.
Pia tumeanzisha mtazamo wa kikanda, kutathmini uwezo wa uzalishaji katika Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda kama vile ECOWAS na SADC.
Je, unashirikishaje nchi hizi?
Tunashirikiana na kila nchi kwa kuhusisha pande zote, na kupitia mashirika ya kikanda kama vile Umoja wa Afrika. Mkakati wetu wa ushirikishwaji unalenga vikwazo maalum vilivyotambuliwa ndani ya kila nchi.
Tunatumia kipimo kinachotegemea takwimu, Kipimo cha Uwezo wa Kuzalisha (PCI), ili kubainisha changamoto. Kwa sababu hiyo, tunatekeleza tathmini ya upungufu ili kutambua vikwazo, fursa na mapungufu. Kulingana na tathmini hii, tunapanga programu ya kina ili kushughulikia masuala muhimu.
Je, mumetathmini athari kamili ya mkakati huu?
Ndiyo, ili kukagua hatua. Programu yetu ya ujasiriamali, kwa mfano, imesaidia wajasiriamali kwa mafanikio, kuwasaidia katika kuendeleza mifano bora ya biashara na kuingia katika sekta mpya.
Nchini Angola, makampuni 30 kati ya 100 ya kibinafsi yamepitia mchakato wetu, na asilimia 85 kati yao wakitoa ripoti kuongezeka kwa mauzo. Zaidi ya hayo, asilimia 72 ya kiwango cha ukuaji wa ajira kila mwaka kimeshuhudiwa katika makampuni haya.
Katika ngazi ya kitaasisi, msaada wetu kwa uwezo wa sekta binafsi wa kuuza bidhaa kama vile asali nje ya nchi umechochea uundaji wa mifumo ya uthibitishaji na miundombinu nchini.
Maabara za Angola sasa zina vifaa vyema zaidi vya kushughulikia uthibitishaji, ikiwemo viwango vya usafi wa mimea, sio tu kwa asali bali pia kwa bidhaa mbalimbali za usindikaji wa mazao ya kilimo.
Je, mkakati huu unawiana vipi na malengo ya Eneo la Biashara Huru Barani Afrika (AfCFTA)?
Mkakati huu unawiana vyema na AfCFTA.
Mkakati wetu unafanya kazi kujenga uwezo wa nchi katika mfumo wa kuongeza thamani. Kwa mfano, ikiwa Angola itazalisha asali lakini haifikii idadi ya mitungi inayohitajika kwa ajili ya upakiaji, nchi nyingine ya Afrika inaweza kuziba pengo hilo.
Bila ushuru au kodi chini ya AfCFTA, nchi hizi zinaweza kufanya biashara, kuchakata, kuthibitisha na kuuza nje bidhaa hizi kwa uhuru.
Biashara ya kimataifa inahusisha nchi nyingi. Kwa hivyo, hamusaidii Angola pekee bali washirika wake wa kibiashara pia?
Ndio, hicho ni kipengele muhimu. Kumbuka, mkakati wetu unajaliza badala ya kuchukua nafasi ya mikakati ya maendeleo ya taifa. Pia inawiana na juhudi pana za Umoja wa Mataifa. Mtazamo wetu unaongozwa na mahitaji kwa kuwa tunafaa kujibu maombi ya nchi kuhusu msaada.
Ushirikiano miongoni mwa nchi mbalimnbali ni muhimu. Wazia kuhusu sekta ya magari, ambapo nchi tofauti zinaweza kuzalisha zana tofautitofauti. Kwa kufanya kazi pamoja na kuimarisha uwezo wao, wanaweza kutengeneza zana zote ndani ya bara la Afrika na kuziuza kwa uhuru chini ya AfCFTA. Hali hii ni sawa kwa sekta ya dawa.
Kwenye Ripoti ya Maendeleo ya Kiuchumi barani Afrika 2023, tulibainisha uwezo wa kiteknolojia wa nchi mbalimbali za Afrika. Kwa safaru huru katika bara zima, nchi mbalimbali zinaweza kutumia uwezo huu kwa pamoja.
Je, umehakikishaje uendelevu wa mkakati huu?
Kwanza kabisa, nchi zinamiliki mkakati huu kikamilifu, na kila nchi lazima ianzishe muundo wake wa utawala uliojitolea, ikijumuisha kamati ya uongozi inayowakilisha wizara zote husika.
Kwa mfano, nchini Angola, kamati hii ina mawaziri kadhaa, wanaowakilisha wizara 23 zinazohusika katika utekelezaji wa programu hii, kamati zinazokutana mara mbili kwa mwaka.
Zaidi ya hayo, kamati ya kiufundi, yenye wajumbe kutoka wizara zote, inasaidia juhudi za utekelezaji.
Pia, wawakilishi wa sekta binafsi, wasomi na mashirika ya kiraia wanashiriki katika mikutano na mashauriano yanayofaa. Mashirika haya ndiyo baadhi ya wadau muhimu nchini.
UNCTAD, kwa pamoja na Taasisi zake za Ubora, miungano ya washirika na mashirika wenza ya Umoja wa Mataifa, yanatoa msaasa wa kiufundi.
Baada ya muda, mkakati huo utakuwa sehemu ya kazi ya kawaida ya wizara za serikali, taasisi za sekta binafsi na mitaala ya vyuo vikuu.
Je, mkakati huu unashughulikia teknolojia ya kijani?
Ndio, bila shaka. Afrika ina madini muhimu kwa kusaidia ulimwengu kugeukia nishati ya kijani
- Bara la Afrika lazima liongeze thamani kwa madini haya badala ya kuyasafirisha nje kama malighafi. Kwa mfano, kutumia nishati ya kijani kusindika kobalti barani Afrika kunafaa kwa mazingira kuliko kuisafirisha kuenda bara lingine kwa ajili ya usindikaji wa kiutumia nishati ya kutoa kaboni. Kwa michakato kama hii, Afrika inapaswa kutumia rasilimali zake nyingi za nishati ya kijani.
- Zaidi ya hayo, Afrika lazima itumie teknolojia ya kijani ili isalie kuwa na ushindani. Hili linazidi kuwa muhimu kwani nchi zinaendelea kupitisha na kutekeleza sera za kushughulikia mabadiliko ya tabianchi, haswa zile zinazotumia sera ya biashara kama nyenzo zao kuu.
- Afrika lazima pia iwekeze katika teknolojia ya kijani ili kupunguza uzalishaji wake wa gesi chafu na kuepuka adhabu wakati wa kuuza nje ya bara.
Je, nchi zinakubali uwezeshaji wa wanawake katika mkakati wako?
Uwezeshaji wa wanawake ni kipengele muhimu cha maendeleo ya kiuchumi. Biashara nyingi zinazoongozwa na wanawake ni sehemu ya programu yetu ya ujasiriamali, ambayo inasaidia kikamilifu uwezeshaji wao.
Uchumi wa sanaa, maarufu barani Afrika kwa sekta kama vile Nollywood, unafaidika sana kwa michango ya wanawake.
Katika sekta kama utalii, ambapo wanawake wanatekeleza jukumu kubwa, tunajitahidi kuhakikisha kuwa wanapata fursa sawa ili kuongeza michango yao kwa uchumi wao wa kitaifa na kwa ustawi wao wenyewe.
Ingawa sekta nyingi za kiuchumi zimesalia kutawaliwa na wanaume, tumetumia suluhisho za kiubunifu ili kuongeza ushiriki wa wanawake.
Uchambuzi wetu unajumuisha kikamilifu mtazamo wa kijinsia na kuzingatia makundi mengine maalum ambayo yanahitaji uangalizi maalum, kama vile vijana. Kwa hivyo, mapendekezo ya sera, yanalenga masuala na mazoea ambayo yanaweza kusaidia kuwawezesha wanawake na makundi yaliyotengwa.
Je, unachukulia nini kuwa matokeo yenye mafanikio kwa bara hili?
Kuna hatua mbili muhimu: -
- Kwanza, Afrika lazima itekeleze AfCFTA kikamilifu. Nchi mbalimbali kwa sasa zinaonisha sera zao na AfCFTA, na ni lazima tuweke kipaumbele kwa utekelezaji wake. Kuchukua fursa inayoletwa na soko kubwa la Afrika kunaweza kuleta mageuzi ya kimuundo.
- Pili, Afrika lazima iongeze thamani kwa malighafi yake, hasa ulimwengu unapotafuta madini muhimu kwa ajili ya kuanza kutumia nishati safi. Hatuwezi kumudu kuendelea kuuza nje madini yanayopatikana kwa kiasi kikubwa barani Afrika kama malighafi.
Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, ninatazamia Afrika itajipanga kuongeza thamani kwa rasilimali hizi, na kuupa ulimwengu pembejeo muhimu ya kuendeleza nishati safi.
Mageuzi haya yataleta ajira nzuri, kuongeza mapato, kuboresha huduma za kijamii na, muhimu zaidi, fursa za ajira za teknolojia bora kwa vijana wetu.
Niko na matumaini.