Sorry, you need to enable JavaScript to visit this website.
Skip to main content

Wito wa kuboresha ajira kwa vijana barani Afrika

Kiswahili

Wito wa kuboresha ajira kwa vijana barani Afrika

Kuwa na wafanyakazi walio na ujuzi kunahitaji kuwepo kwa elimu bora ya msingi
2023-11-02
a man.
.
Wito wa kuboresha ajira kwa vijana barani Afrika.
  1. Play Wito wa kuboresha ajira kwa vijana barani Afrika

Pause

Bara Afrika inapaswa kuboresha viwango vya elimu ya msingi ili kuhakikisha uwepo wa wafanyakazi wenye ujuzi ambao wataunda ajira nyingi na bora zaidi ili kuleta mabadiliko ya kiuchumi barani.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Jinsia, Umaskini na Sera za Kijamii (GPSPD) wa Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (UNECA), Sweta Saxena, alisema kuunda ajira zinazofaa kwa vijana wake ni moja ya changamoto kubwa zinazowakabili watunga sera barani Afrika, akisisitiza kwamba idadi inayozidi kukua ya vijana inahitaji ajira ikiwa Afrika itafaidika kwa ukuaji huu wa idadi ya watu na kukidhi matarajio yake ya maendeleo.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa Kikundi cha Wataalamu wa Sera za Kijamii, ulioandaliwa na GPSPD, Bi. Saxena alisema Afrika ina changamoto katika kuunda ajira kwa vijana.  Alisema kuwa kuna ukosefu wa ujuzi wa kutosha kwa vijana barani Afrika.

Takwimu zinaonyesha kuwa karibu robo ya watoto waliosajiliwa katika shule ya msingi hawakamilishi elimu ya msingi huku chini ya asilimia 50 ya wavulana na wasichana ndiyo inayokamilisha elimu ya chini ya sekondari, ikilinganishwa na karibu asilima 80 katika nchi za Asia Kusini na Marekani Kusini. Kiwango cha usajilishaji katika ngazi ya elimu ya juu ni kibaya zaidi kwa kuwa ni chini ya asilimia 10.

"Viwango vya elimu pia viko chini sana, na kutokana na hayo, vijana barani Afrika wanaingia katika soko rasmi la ajira bila ujuzi unaofaa," Bi. Saxena alisema, akitoa maoni kwamba haishangazi kwamba karibu asilimia 90 ya vijana wanaanza maisha yao katika ajira isiyo rasmi na karibu robo ya biashara inataja ukosefu wa wafanyakazi walio na ujuzi kama miongoni mwa vikwazo kuu.

Changamoto nyingine kubwa barani Afrika ni idadi kubwa ya watu waliopata mafunzo wanaishia kukosa ajira na kufanya kazi katika maeneo ambayo hayahusiani na mafunzo waliyoyapata au kuhamia nchi nyingine, ambayo ni mgao mbovu na upotevu wa rasilimali ambazo zinahitajika katika nchi hizi.

Mkutano wa siku mbili wa Kikundi cha Wataalamu umeunganisha wataalam wa kiufundi kutoka nchi 16 wakiwemo wataalamu kutoka serikalini, wasomi, taasisi za wataalamu na mfumo wa Umoja wa Mataifa kukagua matokeo muhimu ya rasimu ya ripoti, Ajira barani Afrika au Ajira kwa Waafrika. 

Ripoti hiyo inalenga kufahamisha na kuchochea mijadala, kuchangia sera bora, kuwezesha utafiti zaidi, na kutambua mapungufu ya maarifa na takwimu.

Mkutano huo unatoa fursa ya kujadili masuala yanayohusiana na idadi ya watu, elimu na uhamiaji wa ujuzi kwa njia jumuishi ili kuharakisha hatua za ngazi ya kitaifa na kikanda kwa ajili ya kuongeza fursa za ajira kwa vijana wa Afrika.

UNECA inasaidia Nchi Wanachama kupitia jukumu lake la kuitisha mikutano, inaosaidia kubainisha changamoto kuu za pamoja zinazokabili bara la Afrika pamoja na hatua zinazofaa. 

Tume pia inafanya kazi kama chombo cha wataalamu ambacho kinajumuisha kufanya utafiti katika taaluma mbalimbali na uchanganuzi wa changamoto muhimu zinazokabili Nchi Wanachama na Afrika kwa ujumla, pamoja na kuendeleza kujifunza kutoka kwa wengine na maendeleo. 

Zaidi ya hayo, UNECA inatoa ushauri wa sera ya moja kwa moja na usaidizi kwa Nchi Wanachama na hii kwa kawaida inatokana na mikutano na mwingiliano kama vile Mkutano wa Kikundi cha Wataalamu.

Bi. Saxena alisema kuwa mikutano ya vikundi vya wataalam ilikuwa muhimu kwa UNECA kwa kuwa ilichangia Tume hiyo kutimiza jukumu lake kuu la kuendeleza maendeleo ya kiuchumi na kijamii kati ya nchi  zetu wanachama.

Katika ulimwengu wa utandawazi wenye urahisi wa kuhamisha mtaji, bidhaa na huduma, uhamaji wa wafanyakazi walio na ujuzi kuvuka mipaka ya kimataifa ulikuwa ni tokeo la kawaida la umoja wa kimataifa na utaratibu wa uhamiaji. 

Uhamaji huu una manufaa mengi, yakiwemo kutuma fedha nyumbani, uwekezaji, na uhusiano wa kibiashara na nchi wanakohamia lakini hali ilikuwa tofauti barani Afrika.

Alitoa lawama kwamba "kupoteza ujuzi ni jambo la kusikitisha kwa nchi nyingi barani Afrika ambazo tayari zinakabiliwa na tatizo la ukosefu wa wafanyakazi waliotaalamika. Kwa kuwa mafunzo na elimu ya juu inafadhiliwa na bajeti ndogo ya elimu ya umma, nchi maskini za Afrika zinafadhili nchi tajiri kupitia uhamiaji wa wafanyakazi walio na ujuzi wa hali ya juu.”

Uhamiaji unaodhibitiwa ipasavyo unatoa fursa kubwa ya kupunguza changamoto ya uhaba wa kazi kwa wafanyakazi walio na ujuzi barani Afrika na kuleta manufaa ya maendeleo kwa pande zote.

"Kuwa na wafanyakazi walio na ujuzi kunahitaji kuimarisha upatikanaji, na viwango vya elimu ya msingi," Bi. Saxena alisema, akihimiza kutafakari upya elimu chini ya mkataba Mpya wa Kijamii.

.