Bangui - Jamhuri ya Afrika ya Kati ina moja ya viwango vya juu zaidi ya vifo vya akina mama wajawazito duniani, ikiwa na vifo 829 miongoni mwa kina mama100,000 vilivyorekodiwa mwaka 2023.
Nyuma ya takwimu hizi, kuna hali halisi yenye maumivu makubwa: wanawake kujifungua mbali na vituo vya afya, umbali mrefu wa kufikia huduma za afya, uhaba wa rasilimali, na wakati mwingine imani zinazozuia upatikanaji wa huduma za afya.
Kwa mujibu wa takwimu za kitaifa, chini ya asilimia 50 ya wanawake wajawazito huhudhuria mashauriano manne yanayopendekezwa ya huduma ya kabla ya kujifungua, na karibu theluthi moja ya kujifungua bado hufanyika majumbani, jambo linalowaweka akina mama na watoto wachanga katika hatari kubwa.
Ili kukabiliana na changamoto hii, nchi imeipa kipaumbele kutoa huduma bora kwa kila mwanamke bila hatari ya kifedha—kiini cha bima ya afya kwa wote. Mkakati wa nchi wa kupunguza vifo vya akina mama, unalenga kutoa huduma muhimu, ikiwemo mashauriano ya kabla ya kujifungua, kujifungua kwa msaada wa wahudumu wa afya wenye ujuzi, na usimamizi wa matatizo ya kiafya kupitia upatikanaji wa huduma kwa wote bila umaskini kuwa kikwazo.
Mkakati huu ni muhimu katika kuzuia vifo vinavyoweza kuepukika. Unazipa familia fursa ya kuishi maisha yenye afya na husaidia kuimarisha imani ya jamii katika mfumo wa afya, jambo ambalo ni muhimu katika kuwahimiza wanawake kutumia huduma zilizopo.
Kupitia ushirikiano wa WHO na ufadhili kutoka kwa mfadhili mkubwa, serikali imechukua hatua madhubuti za kuboresha afya ya uzazi. Moja ya nguzo kuu za mkakati wa kupunguza vifo vya akina mama ni kutoa mafunzo na kuajiri wakunga wa jamii.
Wakunga hawa, waliochaguliwa na jamii zao, wamekuwa kiungo muhimu kati ya familia na vituo vya afya. Wanatoa taarifa, kuwasindikiza na kuwaongoza wanawake wajawazito hadi wakati wa kujifungua, na kuhakikisha ufuatiliaji baada ya kujifungua.
Pia husaidia kubadilisha tabia kwa kueleza kwa nini huduma ya kabla ya kujifungua na kujifungua kwa msaada wa kitaalamu ni muhimu ili kuepuka matatizo. Wanazipa familia uhakika na kujenga uhusiano unaookoa maisha.
“Wakati mmoja, katikati ya usiku, ilibidi nimsindikize mgonjwa kwa miguu hadi hospitalini, nikiwa tayari kuingilia kati njiani ingehitajika,” anasema Erguine Souhat, mkunga katika mji wa Bria, ulioko katika eneo la kati la nchi. “Tunawafuatilia wanawake tangu mwanzo wa ujauzito hadi kipindi cha baada ya kujifungua, ili mama na mtoto wake waendelee kuwa na afya njema.”
Dkt. Romaric Ghislain Zarambaud Bohy-Ngombet, Mkurugenzi wa Afya ya Familia na Idadi ya Watu katika Wizara ya Afya, anabainisha kuwa “kwetu, vifo vya akina mama ni dharura ya kitaifa. Waziri wa Afya ameweka mwelekeo wazi: kuimarisha ujuzi wa watoa huduma, kuboresha miundombinu ya kiufundi, na kuleta huduma karibu zaidi na jamii. Hivi ndivyo tunavyosonga kuelekea bima ya afya kwa wote.”
“Leo, tuna zaidi ya wakunga 1,200 wanaofanya kazi kikamilifu katika wilaya 32 kati ya wilaya 35 za afya nchini. Wanafanya kazi hasa katika maeneo ya vijijini ambako upatikanaji wa vituo vya afya ni mdogo. Katika maeneo wanakofanya kazi, tunaona kupungua kwa takribani asilimia 30 ya kujifungua majumbani na ongezeko la idadi ya wanawake wanaohudhuria mashauriano ya kabla ya kujifungua,” anasema Dan Mauricette, Mratibu wa Kitaifa wa Wakunga wa Jamii.
Mwaka 2024, WHO ilisaidia kuzipatia takribani wodi 30 za uzazi vifaa vya kitabibu na dawa muhimu ili kuwapatia wanawake wajawazito huduma salama na yenye heshima zaidi. WHO pia iliunga mkono mafunzo ya wakunga wa jamii 300 kuhusu huduma muhimu wakati wa ujauzito, kujifungua na kipindi cha baada ya kujifungua, pamoja na rufaa. Kwa jumla, watoa huduma za afya 64 pia walipatiwa mafunzo ya kutambua hatari za magonjwa ya uzazi ili kuhakikisha huduma bora na kuzuia vifo vinavyoweza kuepukika.
“Kila wodi ya uzazi iliyowezeshwa kwa vifaa, kila mkunga aliyepata mafunzo, inaashiria maisha yanayoweza kuokolewa,” anasema Dkt. Caroline Clarinval, Mwakilishi wa WHO katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. “Lengo letu ni wazi: kila mwanamke, popote anapoishi, aweze kujifungua kwa usalama. Hili linahitaji miongozo inayolingana na mazingira, ujuzi ulioimarishwa, na uhamasishaji endelevu wa jamii.”
Maendeleo haya yanabadilisha maisha. Kwa Albertine Shoura, mama wa watoto watatu, msaada wa mkunga ulikuwa muhimu sana wakati wa ujauzito wake na hasa wakati wa kujifungua. “Niliwahi kujifungua nyumbani na karibu nipoteze maisha yangu pamoja na ya mtoto wangu. Kupitia msaada wa Erguine, niliweza kujifungua salama hospitalini, nikiwa nimezungukwa na huduma sahihi. Namshukuru Mungu na namshukuru Erguine kwa kuokoa maisha yangu na ya mtoto wangu,” anasema.
“Wakati mama anaishi na mtoto wake pia, familia nzima hubaki na matumaini. Natamani kila mwanamke katika nchi yangu apate fursa hii na kwamba kuleta uhai kuwe tukio la furaha, siyo hatari kamwe,” anasema Shoura.

