Afrika inaathiriwa sana na mabadiliko ya tabianchi. Bara hili linaongezeka joto kwa kasi kuliko wastani wa dunia, huku likikabiliwa na madhara makubwa ya mabadiliko ya tabianchi licha ya kuchangia kwa kiwango kidogo zaidi katika uzalishaji wa gesi chafu zinazochochea ongezeko la joto duniani.
Hali hii inaonekana wazi kupitia shinikizo linaloongezeka kwenye rasilimali na mifumo ya maji barani Afrika.
Maji ni msingi wa kilimo, maisha ya wananchi, ikolojia na uzalishaji wa nishati.
Hivyo, athari za mabadiliko ya tabianchi zinazohusiana na maji zinaongeza pengo la maendeleo, kuimarisha ukosefu wa usawa, na kuhatarisha maendeleo endelevu ya bara.
Katika Mkutano wa Vijana wa Baraza la Uchumi na Masuala ya Kijamii la Umoja wa Mataifa (ECOSOC Youth Forum) wa mwaka huu, ambao ni mkutano mkubwa zaidi wa kila mwaka wa Umoja wa Mataifa unaowakutanisha vijana, viongozi wanne wa Afrika wanaojihusisha na masuala ya tabianchi waliongoza mjadala muhimu uliosisitiza nafasi ya vijana wa Afrika katika kuibua na kutekeleza suluhisho za changamoto za tabianchi.
Mchango wao wa mawazo ulionesha jinsi vijana si tu wanavyoitikia changamoto ya mabadiliko ya tabianchi, bali pia wanavyoiunda upya ajenda ya maendeleo kupitia ubunifu, utetezi, na hatua zinazotokana na jamii.
Vijana wa Afrika wanatengeneza njia mpya zenye ujasiri katika uongozi wa masuala ya tabianchi, na kuthibitisha kuwa mustakabali wa hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi unaundwa na maono na dhamira yao thabiti.

