Sorry, you need to enable JavaScript to visit this website.
Skip to main content

Maji ya Afrika ni mustakabali wake. Ni nani atakayeyasimamia?

Maoni
Kiswahili

Maji ya Afrika ni mustakabali wake. Ni nani atakayeyasimamia?

Serikali na wafadhili wameyachukulia maji kama changamoto, badala ya kuona maji kama miundombinu ya uzalishaji inayosimama sawa na barabara, bandari na mtandao wa nishati
2026-05-04
Adobe stock
Share
.
Adobe stock
  1. Play Maji ya Afrika ni mustakabali wake. Ni nani atakayeyasimamia?

Pause

Afrika inashikilia asilimia 9% ya maji safi yanayoweza kurejeshwa duniani, zaidi ya gigawati 600 za uwezo wa nishati ya maji ambao haujatumika, na kati ya asilimia 60% na 65% ya ardhi inayofaa kwa kilimo duniani ambayo bado haijatumiwa. 

Wafanyi kazi wake ndio wachanga zaidi ulimwenguni. Soko lake litafikia watu bilioni 2.5 ifikapo mwaka 2050. 

Kwa pamoja, hivi vinaunda kila sababu ya uzalishaji ambayo mifumo ya maji, nishati na chakula duniani itahitaji katika miongo ijayo. Hili si bara la uhaba. Ni bara la utajiri wa kimkakati. Uamuzi wa Umoja wa Afrika (AU) kuweka mada yake ya mwaka 2026 katika maji na usafi wa mazingira unaashiria kwamba uongozi wa bara hilo uko tayari kulisimamia ipasavyo.

Fikiria jinsi utajiri unaosimamiwa vyema unavyoonekana. Bwawa la Grand Inga nchini DR Congo pekee yake lingeweza kuzalisha mara mbili ya nguvu za Three Gorges huko nchini China na kuendesha viwanda katika Afrika ya Kati, Kusini na Magharibi. 

Mradi wa Maji wa Lesotho Highlands Water Project tayari unathibitisha kwamba miundombinu ya maji ya inayovuka mipaka iliyoundwa na Waafrika inaweza kufanya kazi kwa kiwango kikubwa na kusambazwa kwenye miji mikubwa ya uchumi. 

Kupanua umwagiliaji  kutoka asilimia 3.7% ya ardhi inayofaa kwa kilimo ya Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara (takwimu ya chini kabisa katika nchi zinazoendelea) hadi hata asilimia 10% ndani ya muongo mmoja kungebadilisha usalama wa chakula, kuzalisha mamilioni ya ajira katika mnyororo wa thamani wa kilimo, na kupunguza mfiduo wa bara hilo kwa utofauti wa mvua. 

Kila mojawapo ya uwekezaji unawezekana kutumia ufundi wa Afrika. Uhandisi wake unajulikana. Maji yapo. Ardhi ipo. Nguvu kazi ipo.

Swali ni utawala bora. Kuhusu hili, Afrika lazima iseme ukweli yenyewe: mbinu inayotumika sasa haifikii kiwango cha fursa zilizopo. 

Serikali nyingi na pia wafadhili wameyachukulia maji kama changamoto ya utoaji huduma za kijamii, suala la visima na vyoo vinavyosimamiwa mradi kwa mradi, badala ya kuona maji kama miundombinu ya uzalishaji inayosimama sawa na barabara, bandari na mtandao wa nishati. 

Pampu ya mkono iliyowekwa bila bajeti ya gharama ya matengenezo si maendeleo. Choo cha shimo kilichojengwa bila kuunganishwa na mfumo wa usafi wa mazingira si maendeleo. Hatua hizi zinaweza kuonekana kama mafanikio katika mfumo wa matokeo, lakini hazibadilishi uchumi. Ni vifaa vinavyotumika na kutupwa, si mali za kudumu.

Hili ni jambo wazi. Chini ya nusu ya watu wa Afrika, yaani asilimia 41%, wana maji safi ya kunywa na yanayosimamiwa kwa usalama. 

Watoto wa shule ya msingi wapatao milioni 23 huhudhuria darasa wakiwa na njaa. Takriban Waafrika milioni 429 wanaishi katika umaskini uliokithiri, idadi inayotarajiwa kubaki zaidi ya milioni 400 mwaka 2030. 

Takwimu hizi hazimaanishi Afrika ni bara maskini ya rasilimali. Zinaelezea mfano wa utawala unaoyachukulia maji kama usaidizi badala ya mkakati, na mzunguko wa "jenga, acha, jenga tena" unaotumia mali bila namna ya mifumo ya kudumu.

© Adobe Stock

Mapendekezo yangu

Afrika inaweza kuvunja mzunguko huu, na ninapendekeza mabadiliko matatu ambayo yangebadilisha mwelekeo:

  • Kwanza, kupitisha Usimamizi bora wa Mali za Kimkakati kama mafundisho ya bara. Mabwawa, mitandao ya umwagiliaji, mitambo ya kusafisha maji na mifumo ya maji inayovuka mipakani  ni mali zenye muda wa miaka 50 hadi 100. Zinahitaji uangalizi endelevu wa kitaasisi, si muda wa miaka mitano wa mradi. Zisimamie katika mzunguko wote wa maisha, kuanzia mipango hadi matengenezo na ukarabati, huku ukabiliaji wa mabadiliko ya tabianchi ukizingatiwa katika kila hatua. Mzunguko wa "jenga, acha, jenga tena”, utaisha wakati serikali za Afrika zitakapozichukulia mifumo ya maji kama miundombinu ya kitaifa: kama mali za kudumu za kutunzwa, si miradi ya muda ya kukabidhiwa.

  • Pili, kuzindua upanuzi wa umwagiliaji wa bara zima. Asia Kusini inamwagilia asilimia 41% ya ardhi yake ya kilimo. Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara inamwagilia asilimia 3.7%. Kuziba hata sehemu ndogo ya pengo hilo ndani ya muongo mmoja kungeweza kuzalisha ajira, kujenga uongezaji wa thamani ya kilimo, kuimarisha usalama wa chakula, na kupunguza utegemezi wa chakula kinachoingizwa kutoka nje. Maji bila umwagiliaji si chochote. Ardhi bila maji hailishi mtu yeyote. Umwagiliaji uliosimamiwa vizuri ndio njia ya haraka zaidi kutoka kwa utajiri wa asili hadi thamani ya kiuchumi.

  • Tatu, kujenga utawala wa ushirikiano unaoweza kutekelezwa kwa mabonde yanayoshirikiwa. Asilimia 90% ya maji ya uso wa Afrika huvuka mpaka angalau mmoja wa kitaifa. Nile, Niger, Congo, Zambezi: hii ni mifumo ya kikanda inayohitaji utawala wa kikanda. Afrika tayari ina mifano inayofanya kazi. Shirika la Senegal River Basin Development Organisation limesimamia mfumo wa mipakani wa nchi nne kwa nusu karne. Kazi ni kufanya utawala wa ushirikiano kuwa kawaida, si kama heshima ya kidiplomasia bali kama sharti la kimkakati la utulivu na muunganiko wa kikanda.

Kufadhili mabadiliko haya kunahitaji Afrika kuongoza kwa rasilimali zake wenyewe. Kuziba pengo la usalama wa maji kunahitaji kati ya dola bilioni 50 na bilioni 64 kila mwaka, kulingana na Jopo la ngazi ya Juu la Umoja wa Afrika (AU) na Benki ya Maendeleo ya Afrika mtawalia (AfDB). 

Ufadhili mkubwa zaidi lazima uwe wa kutoka ndani ya nchi za 

Afrika zenyewe: rekebisha ushuru wa maji kwa hatua, linda bajeti za matengenezo, zuia upotevu, na uchukulie uwekezaji wa maji kwa uzito sawa na barabara na mtandao wa nishati. 

Afrika pia lazima ilenge ufadhili wa hali ya hewa wa kimataifa, ambao bara hilo limeutumia kidogo sana, kwa uwekezaji wa maji wa kina. Na serikali za Afrika hazipaswi kuzingatia idhini ya mikataba ya ardhi ya kigeni bila tathmini za lazima za athari za maji. 

Serikali za Afrika zinahitaji kushughulikia usimamizi wa ardhi na utawala kwa njia iliyounganishwa na utawala wa maji. Kila mazao yanayolimwa kwenye shamba la Afrika lililopangwa kwa mgeni na kusafirishwa nje ni uhamisho wa maji ya kawaida nje ya bara, maji ambayo hayakuwahi kupewa bei, hayakuwahi kuhesabiwa, hayakuwahi kusimamiwa. 

Ardhi na maji haviwezi kutenganishwa. Kumtenga mmoja ni kumtenga mwingine.

Dunia itaendeleza maji na ardhi ya Afrika katika miongo ijayo. Mchakato huo tayari unaendelea. Mataifa yenye utajiri zaidi, yanayokabiliwa na changamoto yao vya maji na chakula, yanaelewa hesabu ya utajiri wa Afrika na yanajiweka vizuri ipasavyo. Swali pekee ni kama maendeleo haya yatatokea kwa masharti ya Afrika au ya mtu mwingine.

Niruhusu nimalizie kwa huzuni kidogo. 

Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) hayatafikiwa Afrika ifikapo mwaka 2030. Lazima tuseme ukweli. Lakini kizazi baada ya 2030 kinaweza kurithi kitu tofauti, ikiwa viongozi wa Afrika watachagua sasa kusimamia maji kama ambavyo tayari yapon a umuhimu wake: kama msukumo wa mabadiliko ya kiuchumi, msingi wa amani, na mali muhimu zaidi ambayo bara hili linashikilia kamaamana kwa vizazi vyake vijavyo. 

Maji ya Afrika ni mustakabali wake. Swali ni, je, Afrika itayasimamia, au yatasimamiwa na wengine?

* Cristina Duarte ni Katibu Mkuu Msaidizi wa Ofisi ya Mshauri Maalum wa Afrika.

Share
.
Mshauri Maalumu kuhusu Afrika kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa