Licha ya Afrika kuwa na uwezo mkubwa wa kilimo, bado bara hili linaagiza chakula chenye thamani ya mabilioni ya dola na pia linategemea misaada ya chakula. Dk. Meshack Malo, Naibu Mwakilishi wa Kikanda wa Afrika katika Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), anaeleza changamoto zilizopo na kwa nini teknolojia na vijana vitaamua kama bara litaweza kujilisha lenyewe. Ifuatayo ni mahojiano hayo kwa muhtasari:
Uhaba wa chakula umekuwa changamoto ya muda mrefu katika baadhi ya maeneo ya Afrika. Kwa mtazamo wa FAO, hali ilivyo kwa sasa ina uzito wa namna gani?
Hali tunayotarajia kuona ni dunia isiyo na njaa (Zero Hunger). Tunataka kuhakikisha kwamba kila mwanaume, kila mwanamke na kila mtoto anaweza kupata mlo unaofaa kila siku—chakula cha kutosha kwa wingi na chenye ubora anaoutamani.
Hata hivyo, hali hii bado haijafikiwa barani Afrika kwa sasa. Afrika bado inachukua sehemu kubwa ya msaada wa chakula duniani.
Katika Afrika Mashariki, ukame umeathiri mamilioni ya watu katika miaka ya hivi karibuni. Je, hali ikoje kwa sasa katika eneo hilo?
Afrika Mashariki inakabiliwa na changamoto kubwa hasa ukame. Kanda hii hutumia takribani 20% ya msaada wa chakula duniani kutokana na ukame unaojirudia mara kwa mara unaowaathiri watu walio katika mazingira magumu.
Takribani watu milioni 50 wameathirika. Nchi zilizoathirika zaidi ni Somalia (kwa kiwango kikubwa zaidi), Ethiopia (hasa kusini na mashariki mwa nchi), Kenya (mikoa ya kaskazini na mashariki), Sudan Kusini, na Sudan.
Tunahitaji mifumo ya tahadhari ya mapema ili kupunguza tatizo hili.
Kumekuwa na ukame mfululizo unaoharibu mazao na mifugo katika Pembe ya Afrika. Je, umefanya maendeleo yoyote katika urejeshaji?
Kuna baadhi ya maendeleo nchini Ethiopia kupitia uwekezaji wa muda mrefu unaozidi 10.3% na ongezeko la uzalishaji na tija. Kenya imeanza kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji na kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi.
Hata hivyo, ukichanganya mabadiliko ya tabianchi, ukame na ukosefu wa usalama, vinazidisha hali kuwa mbaya zaidi. Eneo hili lina misimu mizuri ya hali ya hewa, hivyo kama utulivu utapatikana, matatizo mengi yanaweza kutatuliwa.
Je, ni changamoto zipi kuu za usalama wa chakula zinazokabili ukanda wa Afrika Magharibi?
Mabadiliko ya tabianchi, kupanda kwa bei ya chakula na vichocheo vingine vinasababisha watu kuhama kwa wingi, jambo linalosababisha migogoro. Migogoro ndiyo chanzo kikubwa cha uhaba wa chakula katika eneo hili, huku makundi yenye silaha kama Boko Haram yakichangia watu kuhama makazi yao.
Watu wengi waliokimbia hawana uwezo wa kulima, au wanakimbia wakati muhimu wa kilimo. Katika maeneo yenye msimu mmoja wa kupanda, wakihama wakati wa kupanda basi hali yao inakuwa mbaya zaidi.
Nchi za Sahel pia ziko katika hali ya hatari. Mshtuko wowote mdogo unaweza kwa urahisi kupelekea hali ya usalama wa chakula kuelekea pabaya zaidi.
Nchi za Afrika Kusini mwa Afrika zimekumbwa na ukame mkali unaohusishwa na mabadiliko ya tabianchi. Hali hii imeathiri vipi uzalishaji wa kilimo na maisha ya wakazi wa vijijini?
Nchini Madagaska ukame unaweza kuwa na athari kubwa sana.
Namibia na Zimbabwe zina mifugo mingi inayokabiliwa na ukame, hivyo kuathiri maisha ya wananchi. Sehemu za Msumbiji pia zimeathirika.
Ukame pia unaweza kuathiri biashara kwenye ukanda wa Africa Kusini kwa urahisi. Mabadiliko ya tabianchi yameongeza magonjwa ya mifugo na mazao.
Hata hivyo, Tanzania imeweza kuzalisha 235% ya mahitaji yake ya mchele na sasa inauza nje.
Malawi pia imeongeza uzalishaji kutokana na uwekezaji mkubwa.
Nchi za Afrika Kaskazini zinategemea sana uagizaji wa chakula kutoka nje. Je, mshtuko wa bei duniani na usumbufu wa usambazaji umeathiri vipi usalama wa chakula katika eneo hili?
Afrika hutumia kati ya dola bilioni 70 hadi 100 kila mwaka kuagiza chakula kutoka nje, huku ngano ikiwa ya kwanza kwa wingi wa uagizaji, ikifuatiwa na mchele, mahindi na kisha mafuta ya kula.
Unaweza kuona jinsi hata ongezeko dogo la bei duniani linavyoweza kuongeza gharama hizo kwa urahisi, hata kufikia dola bilioni 200—fedha ambazo bara la Afrika halina. Matokeo yake ni kwamba tunalazimika kutegemea msaada wa chakula kutoka nje.
Nchi zinapaswa kushirikiana ili kujitosheleza kwa bidhaa hizi muhimu, ili kuepuka shinikizo la mara kwa mara kwenye akiba ya fedha za kigeni wakati wa misimu ya upungufu wa chakula, pamoja na athari za mfumuko wa bei unaosababishwa na hali hiyo.
Je, nchi barani Afrika zinawekeza vya kutosha katika teknolojia na kilimo cha mashine?
Hapana, bado haitoshi. Hatujafikia viwango vya nchi kama Japani. Vijana barani Afrika hawajihusishi kikamilifu na kilimo, jambo linalomaanisha kuwa ongezeko la tija halipatikani kama inavyotarajiwa.
Hata hivyo, mafanikio yameanza kuonekana katika baadhi ya maeneo. Kwa mfano, Ethiopia na Nigeria zimepiga hatua kupitia huduma za kukodisha matrekta pamoja na matumizi makubwa ya zana za ugani za kidijitali.
Je, Tanzania?
Nchini Tanzania, uwekezaji katika kilimo cha kisasa chenye matumizi ya mitambo umeifanya nchi kujitosheleza kwa chakula na pia kuwa muuzaji mkubwa wa nje wa mchele na mahindi.
Morocco na Misri wako mbele katika eneo hili kwa matumizi ya mashine za kisasa za kilimo, mifumo ya umwagiliaji ya kiotomatiki, na kilimo cha usahihi (precision agriculture).
Kwa ujumla, ujasiriamali wa vijana katika matumizi ya mitambo ya kilimo utakuwa muhimu sana katika kufanikisha maendeleo haya.
Jukumu la mabadiliko ya hali ya hewa lina umuhimu gani katika kuchagiza mazingira ya usalama wa chakula barani Afrika kwa sasa?
Ni jambo la muhimu sana na lina athari kubwa. Tukilinganisha athari za mabadiliko ya tabianchi kwa wakulima katika Marekani, Australia, Asia na Afrika, tunaona kwamba wakulima wa Afrika wanaathirika zaidi kutokana na ukosefu wa teknolojia ya kuwalinda dhidi ya changamoto hizo.
Wakulima wengi barani Afrika bado wanategemea mvua pekee na hawajahamia kwenye kilimo cha umwagiliaji, na pia hakuna kiwango cha kutosha cha matumizi ya mitambo ya kisasa ya kilimo. Hali hii inafanya mifumo ya kilimo isiwe na uwezo wa kustahimili athari za ghafla za tabianchi.
Zaidi ya hapo, upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa—yaani kuelewa ni hali gani ya hewa inayotarajiwa na jinsi itakavyoathiri mazao—unaweza kuongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa wakulima kukabiliana na changamoto hizi na kuboresha ustahimilivu wao.
Afrika ina karibu 60% ya ardhi iliona rotuba isiyolimwa duniani, lakini bara bado inaagiza sehemu kubwa ya chakula chake. Kwa nini ni hivyo?
Kwa bahati mbaya, mtu hawezi kula uwezo. Hii ni hadithi ya Afrika kushindwa kutumia uwezo wake. Rasilimali za maji katika Bonde la Kongo pekee zinaweza kusaidia kubadilisha kilimo katika bara hili.
Sudan Kusini, kwa mfano, ina takriban 80% ya ardhi ya kilimo, lakini kwa sababu ya migogoro, watu wamehamishwa na hawawezi kulima katika hali hio.
Kuna haja ya kupanga vizuri na kuona usalama wa chakula kama suala muhimu la usalama wa taifa. La sivyo, katika miaka ijayo, tunaweza kuona kukata tamaa kutokana na uhaba wa chakula. Katika baadhi ya nchi, kwa mfano katika Afrika Mashariki, ukosefu wa mahindi tayari ni suala kuu wakati wa uchaguzi.
Je, FAO inatekeleza programu gani ili kuimarisha usalama wa chakula na ustahimilivu barani Afrika?
Kazi za FAO barani Afrika zimegawanyika katika maeneo makuu manne:
Kwanza ni kuboresha uzalishaji wa chakula. Pengo la uzalishaji wa chakula bado ni kubwa, hivyo kuongeza uzalishaji ni muhimu ili bara lijitosheleze na kuweza kujilisha lenyewe.
Pili ni kuboresha lishe. Tunahitaji kuhakikisha watu wanapata chakula chenye lishe bora, ikiwemo ulaji wa matunda na mboga kwa wingi zaidi.
Tatu ni kuboresha mazingira. Mabadiliko ya tabianchi ni changamoto kubwa, hivyo ni muhimu kulinda rasilimali za maji, ardhi na misitu ili kudumisha mifumo ya ikolojia ilio imara na yenye afya.
Nne ni kuboresha maisha ya watu. Kilimo kinaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi wa nchi za Afrika.
Aidha, baadhi ya nchi huzalisha mazao ya kuuza nje. Kwa mfano, Ghana huzalisha kakao, Kenya chai, nchi za Afrika Kusini mifugo, na Afrika ya Kati ina rasilimali za uvuvi. Rasilimali hizi zinaweza kuboresha maisha ya wananchi katika bara lote.
Hivyo FAO inaweka mkazo katika mtazamo wa uongezaji wa thamani (value chain approach) ili kuhakikisha kilimo kinachangia zaidi katika uchumi wa nchi za Afrika.
Je, kuna mafanikio yoyote ambapo uwekezaji au sera bora zimeboresha usalama wa chakula?
Kupitia mpango wa “Hand-in-Hand”, unaosaidia utekelezaji wa mipango inayoongozwa na nchi husika, tumeona uwekezaji katika kilimo ukiongezeka, ingawa bado hatujafikia kiwango tunachotarajia.
Sekta binafsi pia inaendelea kuwekeza zaidi katika kilimo, na hii imekuwa kipengele kilichokuwa kinakosekana awali. Kwa sasa kuna ongezeko la uwekezaji kama huu barani Afrika, licha ya changamoto zinazoendelea kujitokeza.
Katika Afrika Mashariki, kumekuwa na ongezeko la uzalishaji wa parachichi (avocado) na mazao ya bustani (horticulture), hali iliyoongeza uzalishaji kwa kiasi kikubwa kwa ajili ya masoko ya nje.
Namibia imefanya vizuri katika uzalishaji wa mifugo, ambayo inachangia takribani theluthi mbili ya uzalishaji wa kilimo nchini humo.
Misri imeanzisha kilimo cha kisasa (precision agriculture), na mwaka 2025 ulikuwa mwaka wa rekodi katika mauzo ya mazao ya kilimo, yakifikia thamani ya zaidi ya dola bilioni 11, sawa na takribani asilimia 24% ya mauzo yote ya nje ya nchi.
Morocco inawekeza kwa kiasi kikubwa katika kilimo kupitia mpango wa “Generation Green”, unaolenga kukuza ajira (vijana na ajira vijijini), kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, na matumizi bora ya maji, pamoja na kuunganisha Uongezaji thamani kwa bidhaa na viwanda vya kilimo. Kwa sasa kilimo kinachangia zaidi ya asilimia 13% ya Pato la Taifa.
Uganda imefanikiwa kudhibiti kilimo chake kinachotegemea mvua na imejitosheleza kwa chakula kama ndizi (matooke), mahindi na mihogo. Chakula huzalishwa ndani ya nchi kwa kiwango kikubwa, huku kilimo cha wakulima wadogo kikiwa msingi wa kujitegemea na hata kuiwezesha nchi kuwa msambazaji wa chakula katika ukanda wa Afrika mashariki.
Kwa ujumla, kuna mafanikio mengi yanayoendeshwa na kizazi kipya cha wakulima, na tunaona pia kuongezeka kwa kilimo cha greenhouse pamoja na mifumo ya umwagiliaji.
Teknolojia na ubunifu—kuanzia zana za kidijitali hadi kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi—vinabadilisha kilimo. Ni ubunifu gani yenye matumaini makubwa unaoibuka barani Afrika?
Afrika itakuwa bara lenye idadi kubwa ya vijana zaidi duniani, lakini bado vijana wengi hawavutiwi na kilimo.
Ninapozuru vyuo vikuu barani Afrika, moja ya malalamiko makubwa ni kwamba hawaoni kilimo kama sekta inayovutia. Wanakihusisha na taswira ya zamani ya wanawake wakilima kwa jembe la mkono, jambo linalofanya kilimo kionekane kisicho na mvuto.
Hata hivyo, sasa teknolojia na ubunifu vinafanya mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo barani Afrika. Kwa hivi sasa utakuta matrekta yanayotumia mifumo ya GPS.
Kwa mfano, Rwanda inaongoza katika matumizi ya ndege zisizo na rubani (drones) kwa ajili ya kunyunyizia mazao, na hili litasaidia kuvutia vijana wengi zaidi kuingia katika sekta hii.
Ubunifu utaendelea kuwa na nafasi muhimu, sambamba na uwekaji wa mitambo ya kisasa (mechanization), na hivyo kuifikisha kilimo katika kiwango kinachotarajiwa. Afrika ilikosa wakati wa Green Revolution, lakini tunatarajia kwamba katika eneo la teknolojia na ubunifu hatutabaki nyuma.
Mifumo ya akili bandia (AI), hata ile rahisi, inaweza kusaidia kuboresha mifugo na kuongeza uzalishaji wa maziwa. Katika baadhi ya nchi, ng’ombe huzalisha lita 1 au 1.5 za maziwa kwa siku, lakini kwa mifumo bora uzalishaji unaweza kufikia hadi lita 15 kwa siku.
Ungependa kuwaambia nini watunga sera, viongozi, washirika wa maendeleo na wawekezaji kuhusu kile kinachohitajika sasa ili kuhakikisha Afrika inajilisha yenyewe na vizazi vijavyo?
Katika miaka ya 1950 na 1960, Afrika ilipigania kwa nguvu uhuru wa kisiasa. Sasa swali ni: je, tunaweza kuelekea uhuru wa chakula? Je, Afrika inaweza kujitoa katika utegemezi wa misaada ya chakula?
Kwa upande wa wasomi na taasisi za utafiti, kuna haja ya kufanya tafiti zaidi kuhusu namna ya kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, pamoja na teknolojia na ubunifu utakaoisaidia Afrika kuendana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Ujumbe wako kwa vijana wa Afrika kuhusu kilimo na kuhakikisha Afrika inajilisha yenyewe ni upi?
Kwa vijana wa Afrika, mchango wenu ni muhimu sana.
Biashara ya chakula itakuwa biashara yenye faida kubwa katika miaka ijayo.
Bara hili bado linatumia zaidi ya dola bilioni 50 kwa mwaka kuagiza chakula, na hili linatoa fursa kubwa kwa vijana kuwekeza katika kilimo na kunufaika na soko ambalo kwa sasa linachukuliwa na nchi zilizo nje ya Afrika.
Vijana wana nafasi kubwa ya kulenga soko hili na hata kunufaika hata kama ni kwa sehemu ndogo tu ya fursa hii.
Kwa ubunifu na nguvu zao, vijana wa Afrika wataweza kubuni njia za kuingia na kunufaika na soko hilo.

