Sorry, you need to enable JavaScript to visit this website.
Skip to main content

Kutoka Azimio hadi Matokeo Halisi: Kuhakikisha Upatikanaji wa Maji na Usafi wa Mazingira kwa Ajili ya “Afrika Tunayoitaka”

Maoni
Kiswahili

Kutoka Azimio hadi Matokeo Halisi: Kuhakikisha Upatikanaji wa Maji na Usafi wa Mazingira kwa Ajili ya “Afrika Tunayoitaka”

2026-03-18
Clean drinking water runs from a faucet in Senegal.
Share
Maji safi ya kunywa yanatoka kwenye bomba nchini Senegal.
UN Photo/Evan Schneider
  1. Play Kutoka Azimio hadi Matokeo Halisi: Kuhakikisha Upatikanaji wa Maji na Usafi wa Mazingira kwa Ajili ya “Afrika Tunayoitaka”

Pause

Umoja wa Afrika umetangaza kaulimbiu ya mwaka 2026 kuwa: “Kuhakikisha Upatikanaji Endelevu wa Maji na Mifumo Salama ya Usafi wa Mazingira ili Kufanikisha malengo ya Agenda 2063.” Kupitia makala hii ya maoni, Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), Mahmoud Ali Youssouf, anaeleza dhamira mpya ya bara la Afrika katika kulinda na kusimamia kwa uendelevu rasilimali zake muhimu za maji.

Viongozi wa nchi na serikali za Afrika walipokutana Addis Ababa tarehe 14 Februari 2026 katika Mkutano wa 39 wa Kawaida wa Umoja wa Afrika, hawakupitisha tu azimio jingine. Walifanya uamuzi muhimu wa kuweka rasilimali ya msingi zaidi kwa maisha na maendeleo ya bara letu “maji” kuwa kitovu cha ajenda yao.

Kaulimbiu waliyoipitisha viongozi wetu, “Kuhakikisha Upatikanaji Endelevu wa Maji na Mifumo Salama ya Usafi wa Mazingira ili Kufanikisha Malengo ya Agenda 2063,” si maneno ya kawaida ya kiutawala. Ni tamko la dhamira linaonesha ukweli kwamba bila usalama wa maji, haiwezekani kuwa na usalama wa chakula, maendeleo ya viwanda, afya bora ya jamii, wala amani na ustawi wa kudumu.

Changamoto tunazokabiliana nazo bado ni kubwa. Katika maeneo mengi ya Afrika, uhaba wa maji na ukosefu wa huduma bora za usafi wa mazingira vinaendelea kudhoofisha ukuaji wa uchumi na utu wa binadamu. Magonjwa yatokanayo na maji machafu bado ni miongoni mwa visababishi vikuu vya vifo. 

Mamilioni ya Waafrika, hasa wanawake na wasichana wa vijijini, bado hutembea umbali mrefu kila siku kutafuta maji badala ya kuhudhuria shule, kujihusisha na shughuli za kiuchumi au kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii zao.

Hili si tatizo la usumbufu pekee; ni ukosefu wa haki. Pia ni kikwazo katika kutimiza malengo ya Agenda 2063, ambayo ni dira ya pamoja ya Afrika ya kufikia maendeleo jumuishi, endelevu na ustawi wa wote.

Mwaka 2026 unapaswa kuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa: kutoka katika kutambua matatizo hadi kuyatatua kwa vitendo.

Idara ya Kilimo, Maendeleo Vijijini, Uchumi wa Buluu na Mazingira Endelevu ya Tume ya Umoja wa Afrika imepewa jukumu la kuratibu utekelezaji wa ajenda hii. Hata hivyo, jukumu hili haliwezi kubebwa na idara moja au Tume ya Umoja wa Afrika pekee. Mafanikio yanahitaji ushirikiano wa nchi wanachama, jumuiya za kikanda, asasi za kiraia, sekta binafsi na muhimu zaidi, wananchi wa Afrika wenyewe.

Dharura ya hatua hizi imeongezwa na athari za mabadiliko ya tabianchi. Afrika tayari inakumbwa na ukame wa mara kwa mara na mafuriko makubwa. Mabadiliko ya mvua yanasababisha mito, maziwa na mabwawa kukauka katika baadhi ya maeneo huku sehemu nyingine zikikumbwa na mafuriko makubwa. Hali hii inahatarisha maisha ya mamilioni ya Waafrika wanaotegemea kilimo na ufugaji.

Kwa hiyo, usimamizi endelevu wa maji si suala la maendeleo pekee, bali pia ni msingi wa kujenga ustahimilivu dhidi ya majanga.

Maji pia yanatufundisha umuhimu wa ushirikiano. Takribani asilimia 60 ya rasilimali za maji safi za Afrika zinashirikiwa kati ya nchi mbali mbali. Mito kama Nile, Niger, Congo, Zambezi na Volta inapita katika mipaka ya nchi nyingi.

Rasilimali hizi zinaweza kuwa chanzo cha ushirikiano au migogoro. Chaguo liko mikononi mwetu. Ni lazima tuimarishe mifumo ya pamoja ya usimamizi wa haki na endelevu wa maji yanayovuka mipaka ya nchi, kwa sababu maji hayatambui mipaka ya kisiasa.

Huduma za usafi wa mazingira nazo zinahitaji kupewa kipaumbele sawa. Usafi salama wa mazingira si anasa bali ni haki ya msingi ya binadamu inayolinda afya, utu na kuongeza uzalishaji wa kiuchumi. 

Hata hivyo, mamilioni ya Waafrika, hasa vijijini na katika makazi ya mijini yanayokua kwa kasi, bado hawana huduma hata za msingi za usafi wa mazingira. Katika karne ya ishirini na moja, hali hii haikubaliki.

Kutatua changamoto hizi kunahitaji uwekezaji mkubwa, ubunifu na dhamira ya kisiasa. Pia kunahitaji mabadiliko katika namna tunavyobuni na kutekeleza suluhisho. 

Maendeleo endelevu hayawezi kulazimishwa kutoka juu; jamii lazima zishirikishwe katika kupanga, kujenga na kusimamia miradi ya maji na usafi wa mazingira. Umiliki wa wananchi ndiyo unaohakikisha miradi hiyo inadumu na kuwanufaisha watu.

Kwa sababu hiyo, Umoja wa Afrika unaandaa mkakati wa kina wa utekelezaji wa kaulimbiu ya mwaka 2026. Mkakati huo utahamasisha matumizi ya teknolojia bunifu za kusafisha maji na kusimamia rasilimali kwa ufanisi, kuimarisha utawala wa sekta ya maji, kupanua huduma za usafi wa mazingira, pamoja na kuhakikisha ushiriki wa vijana, wanawake na makundi yaliyotengwa. Aidha, utawezesha nchi wanachama kubadilishana uzoefu na mbinu bora.

Ubunifu

Ubunifu, ushirikishwaji na ushirikiano vinapaswa kuwa nguzo kuu za juhudi zetu.

Katika ziara zangu mbalimbali barani Afrika kama Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, nimeendelea kushuhudia kwamba maji si suala la miundombinu au sera pekee; ni suala la maisha ya watu.

Ni kuhusu mama anayepata matumaini kwamba mtoto wake hatakufa tena kutokana na ugonjwa unaosababishwa na maji machafu. Ni kuhusu msichana anayebaki shuleni kwa sababu kijiji chake kina maji safi. Ni kuhusu mkulima anayemwagilia maji mazao yake wakati wa ukame. Ni kuhusu mfanyabiashara anayepanua biashara yake kwa sababu kuna huduma ya uhakika ya maji.

Mabadiliko haya ya kila siku ndiyo msingi halisi wa maendeleo ya Afrika.

Kwa hiyo, kaulimbiu ya Umoja wa Afrika kwa mwaka 2026 ni wito kwa serikali zote kuweka sekta ya maji na usafi wa mazingira katika kipaumbele cha mipango yao ya maendeleo. Kwa kuwa maji yanagusa sekta zote; kilimo, afya, nishati, viwanda na elimu—majibu yetu nayo lazima yawe ya pamoja na yaliyounganishwa.

Nchi za Afrika zinapaswa kuimarisha ushirikiano, kubadilishana utaalamu na kuhamasisha rasilimali kwa ajili ya kukabiliana na changamoto hizi. 

Jumuiya za kikanda na taasisi za usimamizi wa mabonde ya mito zina nafasi muhimu katika kuimarisha usimamizi wa pamoja wa rasilimali za maji. 

Umoja wa Afrika utaendelea kuratibu mazungumzo na ushirikiano unaolenga usimamizi wa haki na endelevu wa maji yanayoshirikiwa.

Hata hivyo, serikali haziwezi kufanya kila kitu peke yake. Asasi za kiraia, sekta binafsi, taasisi za utafiti na washirika wa maendeleo lazima pia wachangie utaalamu na rasilimali zao. 

Uwekezaji katika miundombinu ya maji, huduma za usafi wa mazingira na usimamizi wa maji unaozingatia mabadiliko ya tabianchi ni uwekezaji katika amani, ustawi na mustakabali wa Afrika.

Hatari na fursa ziko wazi. Kufikia mwaka 2050, idadi ya watu barani Afrika inatarajiwa kuongezeka maradufu, hali itakayoongeza mahitaji ya maji na miundombinu. Hatua tunazochukua leo ndizo zitaamua kama miji yetu itastawi, kilimo chetu kitaweza kulisha watu wetu, na uchumi wetu utafikia uwezo wake kamili.

Ndiyo maana kaulimbiu ya Umoja wa Afrika kwa mwaka 2026 si kauli mbiu tu; ni ahadi ya pamoja ya bara letu.

Kwa pamoja tunaweza kuhakikisha kila Mwafrika anapata maji salama na huduma bora za usafi wa mazingira. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa si tu tunaokoa maisha na kuboresha ustawi wa wananchi, bali pia tunafungua milango ya maendeleo endelevu katika bara lote.

Mwisho wa yote, mafanikio yetu hayatapimwa kwa uzuri wa matamshi yetu au idadi ya maazimio tunayopitisha. Yatapimwa kwa mabomba yanayotoa maji, mifumo ya usafi wa mazingira inayofanya kazi ipasavyo, na mamilioni ya maisha ya Waafrika yatakayobadilika kuwa bora.

Share
.
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika