Wakati FAO ikiratibu utekelezaji wa Mwaka wa Kimataifa wa Mkulima Mwanamke 2026, kiongozi wa timu ya masuala ya kijinsia Tacko Ndiaye anaeleza kwa nini kuwekeza kwa wakulima wanawake wa Afrika ni jambo la lazima kwa usalama wa chakula, ukuaji wa uchumi na kujenga mifumo imara zaidi ya kilimo na chakula
Africa Renewal: Wakulima wanawake wana nafasi gani katika kuhakikisha usalama wa chakula barani Afrika?
Bi. Ndiaye: Tunafahamu kuwa wanawake ndio moyo wa mifumo ya kilimo na chakula barani Afrika. Kote katika bara hili, wanawake wana nafasi kuu katika mifumo ya kilimo na chakula kupitia nguvu kazi yao, utaalamu wao na shughuli zao za utunzaji, wakizihudumia kaya, jamii na masoko ya ndani.
Wanawake ni takriban nusu ya nguvu kazi ya kilimo na chakula - asilimia 49 - na wanachangia katika kila hatua ya mnyororo wa thamani, kuanzia uzalishaji na usindikaji hadi usambazaji na biashara, kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya FAO, Hali ya Wanawake katika Mifumo ya Kilimo na Chakula Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Aidha, wanawake ni walinzi wa utamaduni na wahifadhi wa maarifa asilia yaliyorithishwa kizazi hadi kizazi kuhusu uhifadhi wa mbegu na ulinzi wa bioanuwai, pamoja na kudumisha mafungamano ya kijamii yanayoshikilia sekta ya kilimo na chakula.
Wakati huo huo, Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara inaendelea kukabiliwa na changamoto lukuki za ukosefu wa usalama wa chakula. Kwa mfano, mwaka 2024, takriban asilimia 64 ya wakazi wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara walikumbwa na ukosefu wa usalama wa chakula wa kiwango cha wastani au kikubwa, kwa mujibu wa takwimu za FAO. Pia tunajua kuwa zaidi ya asilimia 30 ya wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49 katika ukanda huu wanakabiliwa na upungufu wa damu.
Iwapo Afrika inataka kukabiliana na changamoto zake za usalama wa chakula, kuwawezesha wakulima wanawake lazima kuwe kipaumbele.
Ni changamoto zipi kubwa zaidi zinazowakabili wakulima wanawake barani Afrika leo?
Barani Afrika, kama unavyojua, wanawake ndio wanaolima ardhi. Kila unapoona chapisho kuhusu kilimo na mifumo ya chakula barani Afrika, uwezekano ni mkubwa kuwa utaona picha ya mkulima mwanamke ukurasa wa mbele.
Hata hivyo, licha ya nafasi yao kuu, wanawake wanaendelea kukabiliwa na ukosefu wa usawa wa kimuundo unaopunguza tija yao, ustahimilivu wao na fursa zao za kiuchumi.
- Kikwazo kimojawapo kikubwa zaidi kwa wanawake ni ukosefu wa usawa katika kupata na kumiliki ardhi. Katika nchi 28 kati ya 32 za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara tulizozifanyia utafiti, wanaume wana uwezekano mkubwa zaidi kuliko wanawake wa kumiliki au kudhibiti ardhi ya kilimo. Katika zaidi ya asilimia 40 ya nchi hizo, pengo la kijinsia katika umiliki au haki za uhakika juu ya ardhi ya kilimo ni kubwa mno.
- Pia tunajua kuwa hata pale ambapo kuna sheria ya kulinda haki za ardhi, ulinzi huo wa kisheria ni dhaifu au hautoshi. Katika nusu ya nchi tulizozichunguza, sheria hazilindi ipasavyo haki za ardhi za wanawake.
- Umiliki wa ardhi pia unahusiana kwa karibu na upatikanaji wa huduma za kifedha kwa sababu ardhi mara nyingi hutumika kama dhamana. Hata hivyo ni asilimia 49 tu ya wanawake katika ukanda huu wanaomiliki akaunti ya kifedha, ikilinganishwa na asilimia 61 ya wanaume.
- Wanawake pia wanakabiliwa na vikwazo vya kupata pembejeo za kilimo, huduma za ugani, masoko na teknolojia.
- Kutengwa kidijitali ni changamoto nyingine. Mifumo ya kidijitali imekuwa muhimu kwa kuuza bidhaa, kupata taarifa na kujifunza ujuzi mpya. Hata hivyo, uwezekano wa wanawake kutumia intaneti ya simu ni mdogo kwa asilimia 29 ikilinganishwa na wanaume. Inakadiriwa kuwa wanawake milioni 205 katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara bado hawana fursa ya kutumia zana za kidijitali.
- Zaidi ya hayo, licha ya mchango wao mkubwa katika mifumo ya kilimo na chakula, wanawake mara nyingi hufanya kazi katika mazingira duni kuliko wanaume. Wamejikita zaidi katika ajira zisizo na uhakika, zisizo rasmi, zinazotegemea nguvu kazi kubwa, zenye ujuzi mdogo na malipo duni. Hili linadhihirika katika ukweli kwamba takriban asilimia 90 ya wanawake katika ukanda huu wanafanya kazi katika sekta isiyo rasmi.
- Mila na desturi za kibaguzi, ukatili wa kijinsia, vizuizi dhidi ya uongozi na ushiriki wa wanawake, na mzigo mkubwa wa kazi za utunzaji zisizolipwa vinapunguza zaidi fursa zao.
Kuna changamoto nyingi zinazopaswa kushughulikiwa iwapo tunataka kujenga mifumo ya kilimo na chakula iliyo shirikishi zaidi, imara zaidi na yenye ufanisi zaidi.

Je, unaona vijana, hasa wanawake vijana, wakionesha nia ya kujihusisha na kilimo?
Vijana barani Afrika, kama ilivyo kwingineko, huvutiwa na ubunifu na fursa zenye mvuto na uhai. Changamoto ni jinsi ya kukifanya kilimo kiwe cha kuvutia zaidi na chenye maana zaidi kwa ndoto zao.
Wanawake vijana wanakabiliwa na vikwazo vya kipekee. Mara nyingi wanahangaika kupata ardhi kwa sababu ya sheria za urithi na mila za kijamii. Lakini pia wanakabiliwa na vikwazo vya ziada vinavyotokana na jinsia.
Vijana wengi wa Kiafrika bado wanakiangalia kilimo kwa mtazamo wa zamani. Swali ni: Tunawezaje kukifanya kilimo kionekane cha "kisasa" na cha kuvutia?
Tunawezaje kutumia nguvu, ubunifu na ari ya ujasiriamali ya vijana? Tunawezaje kuwavutia vijana? Teknolojia mpya, zana za kidijitali, kilimo himilivu kwa mabadiliko ya tabianchi na ubunifu vinaweza kusaidia kubadili mitazamo na kuunda fursa mpya.
Hivi karibuni nilizungumza na kiongozi mwanamke ambaye jamii yake inachanganya kilimo na utalii ikolojia. Wanawake wanajikita katika uzalishaji wa kilimo, huku vijana wakishiriki katika shughuli za utalii ikolojia. Mtazamo huu hauzalishi tu vipato, bali pia unahimiza uhifadhi wa bioanuwai na ulinzi wa urithi wa kilimo na chakula. Ubunifu wa aina hii unaweza kusaidia kuwavutia vijana katika sekta hii.
Wanawake vijana wanaendelea kukabiliwa na changamoto zinazohusiana na ardhi, fedha, maarifa na ufanyaji maamuzi. Kuna nafasi kubwa ya kufanya mageuzi ya mila, sheria na desturi zinazowanyima haki.
Tunahitaji kuunda fursa zaidi kwa vijana katika mifumo ya kilimo na chakula - si ajira tu, bali ajira zenye staha, zenye mishahara ya haki, mazingira bora ya kazi na fursa za uongozi. Vijana pia lazima wawe na sauti yenye nguvu zaidi katika kutunga sera na katika michakato ya mageuzi ya mifumo ya kilimo na chakula.
FAO ilizindua Mwaka wa Kimataifa wa Mkulima Mwanamke (IYWF) 2026. Mpango huu unahusu nini na malengo yake ni yapi?
Mwaka wa Kimataifa wa Mkulima Mwanamke 2026 ulitangazwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambalo liliitaka FAO, kwa kushirikiana na IFAD na WFP, kuongoza maadhimisho ya kimataifa. Zaidi ya nchi 120 zilidhamini kwa pamoja azimio hilo.
Kama FAO, sisi ndio wenyeji wa Sekretarieti na tunaratibu juhudi za kimataifa. Mwaka huu unajibu utambuzi uliochelewa lakini wa kihistoria: wanawake ni muhimu kwa mifumo ya kilimo na chakula. Wanalima, wanasindika, wanasambaza na wanafanya biashara ya chakula; wanachangia usalama wa chakula na lishe katika kaya; na wanafanya kazi muhimu za utunzaji zinazoendeleza jamii za vijijini.
Kwa ufupi, mifumo ya kilimo na chakula isingefanya kazi bila wanawake.
Hata hivyo, michango ya wanawake bado mara nyingi hutolewa bila haki za uhakika juu ya ardhi na maliasili, bila fursa sawa za kupata huduma za kifedha, masoko, huduma nyingine na teknolojia, na bila sauti sawa katika ufanyaji maamuzi.
Kwa hivyo Mwaka huu wa Kimataifa ni fursa na wito wa kuchukua hatua kwa wakati mmoja: kuwatambua na kuwaenzi wakulima wanawake, huku tukishughulikia vikwazo vinavyozuia uwezo wao.
Malengo yake yamejengwa kwenye vipaumbele sita: kuongeza uelewa wa umma kuhusu nafasi za wanawake; kuimarisha umakini kwenye umiliki wa ardhi na haki za wanawake za ardhi; kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha, bima na masoko; kupanua upatikanaji wa huduma za ushauri, elimu na teknolojia; kuhamasisha sera na uwekezaji unaozingatia jinsia; na kujenga ushirikiano baina ya mipango ya kimataifa ili maendeleo yaendelee hata baada ya mwaka 2026.
Hatimaye, kwa kukuza usawa wa kijinsia na kuweka mazingira yanayowawezesha wanawake wanaoshiriki katika minyororo yote ya thamani ya kilimo na chakula kustawi, Mwaka huu wa Kimataifa unachangia kujenga mifumo ya kilimo na chakula iliyo ya haki zaidi, shirikishi zaidi na endelevu kwa wote.
Zaidi ya sera na utetezi, unaweza kutupa mifano ya mipango ya vitendo ambayo FAO inatekeleza kupambana na njaa na kuboresha usalama wa chakula?
FAO inaunga mkono mipango kadhaa ya vitendo inayoongozwa na jamii ambayo inasaidia watu kuzalisha chakula zaidi, kuongeza vipato vyao na kujenga ustahimilivu dhidi ya misukosuko ya tabianchi na kiuchumi.
- Mojawapo ya mipango yenye mafanikio makubwa ni programu ya "Shule za Wakulima Shambani" (Farmer Field Schools - FFS), ambapo wakulima hujifunza kwa kutenda. Shule hizi huwapa wakulima ujuzi wa vitendo wa kuongeza tija, kutatua changamoto za ndani na kukabiliana na mabadiliko ya mazingira. Kati ya mwaka 2024 na 2025, takriban shule 29,000 za wakulima shambani zilikuwa zikiendeshwa katika nchi 86. Shule hizi pia zinahimiza ushiriki wa dhati wa wanawake, vijana na makundi yaliyotengwa. FAO iliandaa Mwongozo wa Kuingiza Masuala ya Kijinsia katika Shule za Wakulima Shambani: Kuelekea Programu Zinazoleta Mageuzi ya Kijinsia, na kwa sasa inaandaa nyenzo za ziada za mafunzo ili kuwasaidia watekelezaji kuingiza mikabala inayozingatia jinsia na inayoleta mageuzi ya kijinsia katika mzunguko mzima wa FFS.
- Mfano mwingine ni "Vilabu vya Dimitra." Hivi ni vikundi vinavyoongozwa na jamii ambapo wanawake, wanaume na vijana hukutana kujadili changamoto za pamoja, kubaini suluhisho za vitendo na kuchukua hatua za pamoja ili kuboresha jamii zao, maisha yao na ustawi wao. Kufikia Mei 2026, kulikuwa na zaidi ya vilabu 11,000 vya Dimitra vilivyokuwa hai katika nchi 20, vikiwakutanisha wanachama zaidi ya 330,000. Zaidi ya kuboresha maisha na usalama wa chakula, vilabu hivi vinasaidia kubadili mila na desturi za kijamii na kuimarisha sauti na uongozi wa wanawake.
- Kisha kuna Programu ya Pamoja ya Kuharakisha Maendeleo Kuelekea Uwezeshaji wa Kiuchumi wa Wanawake Vijijini (JP RWEE). Ikitekelezwa na FAO, IFAD, WFP na UN Women, programu hii inawasaidia wanawake wa vijijini kupata huduma za kifedha, pamoja na mafunzo ya kilimo, ujasiriamali, uongozi, lishe na ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Awamu ya kwanza (2014–2021), iliyotekelezwa katika nchi saba ikiwemo Ethiopia, Liberia, Niger na Rwanda, iliwafikia wanawake zaidi ya 80,000 wa vijijini na kunufaisha kaya zaidi ya 400,000. Wanawake washiriki walirekodi ongezeko la wastani wa asilimia 82 la uzalishaji, walipata mauzo ya zaidi ya dola milioni 3.6, walikusanya dola milioni 1.9 kupitia vikundi vya akiba na mikopo, na wanawake zaidi ya 40,000 walipata mafunzo ya kilimo.
Nchini Ethiopia, kwa mfano, programu ilisaidia kufungua fursa za kupata huduma za kifedha kupitia vyama vya ushirika vya akiba na mikopo vya wanawake, ambavyo navyo vilifungua fursa ya kupata mbegu bora, pampu za maji, mabomba na vifaa, pamoja na mifugo midogo kwa ajili ya kuzalisha na kunenepesha, sambamba na kituo maalum cha mafunzo ya wakulima.
Programu kwa sasa iko katika awamu yake ya pili (2022-2027), ikiendeshwa nchini Nepal, Niger, Tanzania, Tunisia na Visiwa vya Pasifiki, ikiwa na msisitizo mkubwa zaidi kwenye ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

